• Nairobi
  • Last Updated February 29th, 2024 5:56 PM
Man-City sasa yatangazia Arsenal hali ya hatari EPL

Man-City sasa yatangazia Arsenal hali ya hatari EPL

NA MASHIRIKA

KOCHA Pep Guardiola ametaka masogora wake kusakata mechi ijayo ya Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) dhidi ya Arsenal kama fainali.

Hii ni baada ya viongozi wa EPL kushindwa kuruka kamba ya West Ham licha ya kutwaa uongozi kipindi cha kwanza, uwanjani London Stadium, jana Jumapili.

Arsenal waliwekwa kifua mbele na Gabriel Jesus na nahodha Martin Odegaard.

Lakini West Ham walizinduka kabla mapumziko kwa penalti ya Said Benrahma kabla Jarrod Bowen kusawazisha mambo kipindi cha pili.

Arsenal watajilaumu kutupa alama mbili muhimu kileleni kwani wana alama 74 huku miamba Man-City wakiwa na 70 pamoja na mechi moja ya akiba.

Miamba hao kukomoa Leicester City 3-1 mnamo Jumamosi uwanjani Etihad, na kuweka hai matumaini ya kujizolea mataji matatu muhula huu, ikiwemo kuhifadhi ufalme wa EPL.

Man-City watarudiana na Bayern Munich robo-fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) Jumatano nchini Ujerumani.

Kisha kuvaana na Sheffield United katika nusu-fainali ya Kombe la FA mnamo Aprili 22. Baada ya hapo, wataalika Arsenal pambano la kufa kupona ligini Aprili 26.

Huku wakitarajiwa kufuzu rahisi kwa nusu-fainali ya UEFA na fainali ya FA, mechi dhidi ya Gunners katika EPL itachangia pakubwa kuamua iwapo Man-City watahifadhi ligi au la.

“Ni kushinda, kushinda na kushinda tu. Arsenal wamekuwa na msimu wa kuridhisha sana na sidhani watakuwa wepesi kuangushwa,” alitanguliza Guardiola baada ya mechi ya Jumamosi ugani Etihad.

“Ushindi dhidi ya Leicester unatupa motisha na tutapata nguvu zaidi ya kuwakomoa iwapo tutatinga nne-bora UEFA na kuingia fainali ya FA kabla ya fainali hiyo,” akaongeza kocha huyo Mhispania.

Akicheza dhidi ya Leicester, fowadi matata Erling Haaland alifunga mabao mawili na kufikisha magoli 47 kapuni mwake kutokana na mechi 40 za mashindano yote msimu huu.

Raia huyo wa Norway ana mabao 32 EPL akivalia jezi ya Man-City na analenga kuvunja rekodi za vigogo Alan Shearer na Andy Cole waliotinga magoli 34 msimu mmoja ligini.

Huku Man-City wakitamba, masaibu ya Chelsea ligini yaliendelezwa na Brighton waliotoka nyuma na kuwalima 2-1 uwanjani Stamford Bridge.

Ilikuwa mara ya kwanza Chelsea kupoteza dhidi ya Brighton nyumbani katika historia.

Pengo la pointi 10 linatenganisha Chelsea na nambari saba Brighton, wanaofukuzia fursa ya kunogesha soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Miamba wengine walioduwazwa katika EPL mnamo Jumamosi ni Tottenham Hotspur, waliotandikwa 3-2 na Bournemouth nyumbani.
Newcastle pia walinyolewa bila maji wakitoa ndani mabao 3-0 na Aston Villa ugenini.

Leo Jumatatu ni zamu ya Leeds United kualika Liverpool, wanaokamata nafasi ya nane ligini kwa alama 44 baada ya mechi 29.

  • Tags

You can share this post!

Ruto: Kalonzo alikataa kuingia boksi

MAPISHI KIKWETU: Pilipili ya limau kwa kuku choma huongeza...

T L