• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 5:55 AM
Man-City waendea ‘Nyundo’

Man-City waendea ‘Nyundo’

NA MASHIRIKA

MANCHESTER City na West Ham watakutana kwa mara ya 120 Ligi Kuu ya Uingereza itakaporejea leo Jumamosi baada ya majukumu ya kitaifa, huku vijana wa kocha Pep Guardiola wakipigiwa upatu wa kuponyoka na ushindi.

West Ham, ambao wako nyumbai ugani London Stadium, wana ushindi 38, sare 19 na vichapo 62 dhidi ya bingwa mtetezi Man-City.

Wote wataingia mechi ya raundi ya tano bila kupoteza nne za kwanza. Viongozi Man-City wameandikisha ushindi mara nne mfululizo nao West Ham, maarufu Hammers, wameshangaza kwa kutawala mechi tatu na kutoka sare moja. Hususan ikizingatiwa kuwa waliuza nyota Declan Rice na pia kuponea tundu la sindano kushushwa ngazi msimu uliopita 2022-2023.

Man-City, ambao wanajivunia kuwa na mfungaji bora msimu uliopita Erling Haaland, wataingia mechi hii na hofu ya majeraha kwa wachezaji watatu.

Jack Grealish alijiondoa kuwakilisha Uingereza katika michuano ya kufuzu Kombe la Bara Ulaya (Euro) 2024 akiwa na jeraha la paja, ingawa si baya hivyo kuna matumaini atatumiwa. John Stones pia hakuhusishwa katika timu ya Uingereza akiwa na jeraha sawa na Grealish. Stones hajachezea City ligini msimu huu naye Grealish alikosa ushindi wa 5-1 dhidi ya Fulham.

Mateo Kovacic pia alikuwa nje Croatia ikilemea Armenia 1-0 katika mechi ya kufuzu kushiriki Euro2024 hapo Septemba 11, ingawa inaaminika hakutumiwa kwa sababu ya tahadhari. Guardiola naye alirejea Jumatano baada ya upasuaji wa mgongo.

Man-City itakutana na Lucas Paqueta, ambaye walijaribu kumsaini bila mafanikio kabla ya soko kufungwa Septemba 1.

West Ham almaarufu Hammers huenda wakampa sajili mpya Konstantinos Mavropanos nafasi leo. Mavropanos amekuwa na jeraha la mgongo. Wazoefu Vladimir Coufal na Tomas Soucek pia watafanyiwa uchunguzi wa kiafya kabla ya mechi hiyo.

Mchuano utakaofungua siku ni kati ya Wolves (nambari 15) na Liverpool (tatu) ugani Molineux. Vijana wa Jurgen Klopp watakuwa makini kuepuka kipigo cha wenyeji wao baada ya kulimwa 3-0 mnamo Februari 4.

Difenda Virgil van Dijk bado anatumikia marufuku baada ya kulishwa kadi nyekundu dhidi ya Newcastle. Mohammed Salah na Darwin Nunez watategemewa kuvamia ngome ya Wolves, ambao nao wanajivunia wavamizi matata Pedro Neto na HeeChan Hwang.

  • Tags

You can share this post!

Hunter amweka babake Rais Biden wa Amerika pabaya kwa...

Kenya Lionesses kikaangioni dhidi ya Afrika Kusini

T L