• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 5:55 AM
Man U wafufuka, majirani zao Man City wakififia EPL

Man U wafufuka, majirani zao Man City wakififia EPL

MANCHESTER, Uingereza

Mabingwa watetezi Manchester City wanaendelea kuona taji likiwaponyoka baada ya kupoteza 1-0 mikononi mwa Aston Villa kwenye Ligi Kuu ya Uingereza, Jumatano.

Katika siku ambayo pia majirani Manchester United walipepeta Chelsea 2-1 na kuongezea masaibu ya kocha Mauricio Pochettino, nao Liverpool wakazidisha presha dhidi ya viongozi Arsenal kwa kukung’uta wavuta-mkia Sheffield United 2-0, City walinyamazishwa na vijana wa Unai Emery kupitia bao la Leon Bailey dakika ya 74.

Villa, ambao watakamatana na wanabunduki wa Arsenal Jumamosi, walizidia City maarifa kabisa na kufanikiwa kuweka mshambulizi Erling Haaland kimya.

Sasa, Villa wameshinda mara 14 mfululizo ugani mwao Villa Park ligini na kufikia rekodi yao ya mwaka 1903 na 1931.

Ushindi huo wa kwanza wa Villa dhidi ya City tangu Septemba 2013 unawainua nafasi moja hadi nambari tatu na kusukuma vijana wa kocha Pep Guardiola katika nafasi ya nne.

Ni mara ya kwanza City wamekosa ushindi ligini mara nne mfululizo tangu Machi-Aprili 2017.

Guardiola aliyejiunga na City mnamo Julai 2016 hadi Juni 2025, alikiri kuwa hawakustahili kupata alama dhidi ya Villa.

“Hatukupiga pasi nzuri na pia hatukujituma vilivyo. Timu nzuri ilishinda,” aliongeza Guardiola ambaye vijana wake walitoka sare dhidi ya Chelsea, Liverpool na Tottenham kabla ya kichapo ugani Villa.

Liverpool ya kocha Jurgen Klopp ilinyonga Sheffield kupitia mabao ya Virgil van Dijk na Dominik Szoboszlai na kukata uongozi wa pointi tano wa Arsenal hadi mbili.

Arsenal wanaongoza kwa alama 36, wakifuatiwa na Liverpool (34) na Villa (32). Villa wako katika nafasi yao nzuri kabisa katika historia ya ligi hiyo tangu watawale msimu 1980/81.

United walipoteza penalti wakilipua Chelsea kupitia mabao ya Scott McTominay. Bruno Fernandes alipoteza penalti dakika ya tisa kabla ya McTominay kufungua ukurasa wa magoli dakika 10 baadaye.

Ingawa Cole Palmer alisawazishia Chelsea kabla ya mapumziko, McTominay alihakikishia wenyeji ushindi alipoongeza bao la pili dakika ya 69 ugani Old Trafford.

Matokeo (Desemba 6): Sheffield United 0-2 Liverpool, Fulham 5-0 Nottingham Forest, Crystal Palace 0-2 Bournemouth, Brighton 2-1 Brentford, Manchester United 2-1 Chelsea, Aston Villa 1-0 Manchester City

  • Tags

You can share this post!

Harambee Starlets warejea kimya kimya baada ya kukosa fursa...

Mzee aliyeoa msichana wa miaka 16 ashtakiwa kwa unajisi

T L