• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Man-United, Man-City na Chelsea kusambaratisha Dortmund iwapo watasajili Sancho, Haaland na Bellingham mtawalia

Man-United, Man-City na Chelsea kusambaratisha Dortmund iwapo watasajili Sancho, Haaland na Bellingham mtawalia

Na MASHIRIKA

MIAMBA wa soka ya Uingereza – Manchester City, Chelsea na Manchester United wako radhi kusambaratisha uthabiti wa Borussia Dortmund kwa kusajili wanasoka watatu tegemeo wa kikosi hicho cha Ligi Kuu ya Ujerumani (Bundesliga) mwishoni mwa kampeni za msimu huu wa 2020-21.

Huku Man-United wakifukuzia huduma za Jadon Sancho ambaye thamani yake ni Sh15 bilioni, Chelsea wako radhi kuweka mezani kima cha Sh14 bilioni ili kujinasia maarifa ya chipukizi Jude Bellingham kutoka Dortmund.

Man-City nao wako tayari kuvunja benki ili kumtwaa fowadi chipukizi raia wa Norway, Erling Braut Haaland ili kujaza pengo la Sergio Aguero ambaye ataagana na kikosi hicho cha kocha Pep Guardiola mwishoni mwa msimu huu.

Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba Aguero ambaye ni raia wa Argentina, huenda akatua Barcelona.

Licha ya makali ya Aguero kushuka pakubwa msimu huu, huduma zake bado zinawaniwa pia na Real Madrid, Juventus, Chelsea na Paris Saint-Germain (PSG).

Akiwa na umri wa miaka 32 pekee, Aguero angali na miaka kadhaa ya kusakata soka yenye ushindani mkali kitaaluma na rekodi yake ya mabao 257 kutokana na mechi 384 inajisemea mengi kuhusu uwezo wake uwanjani.

Haitakuwa ajabu kuona Aguero akitua Barcelona ikizingatiwa kwamba rais mpya wa kikosi hicho, Joan Laporta, aliwahi kuapa kwamba atamsajili sogora huyo iwapo atachaguliwa kuwa rais.

Kubwa zaidi katika mipango ya Laporta ni kumsajili Aguero ili ashirikiane na Lionel Messi katika safu ya mbele ya Barcelona sawa na jinsi ambavyo wawili hao wamekuwa wakifanya katika timu ya taifa ya Argentina.

Aidha, Aguero na Messi wamekuwa marafiki wa karibu sana tangu utotoni na ujio wake uwanjani Camp Nou utamfanya kuwa kizibo cha Luis Suarez aliyeyoyomea Atletico Madrid mwanzoni mwa msimu huu wa 2020-21.

Haaland anayewaniwa pia na vikosi vingi vya haiba kubwa barani Ulaya, anapigiwa upatu wa kutua Man-City baada ya kufungia Dortmund jumla ya mabao 35 kutokana na mechi 32 pekee.

Katika hatua ya kimakusudi inayolenga kutamausha Man-City katika azimio lao la kumsajili Haaland, Dortmund hata hivyo wamefichua kwamba yeyote anayetaka kumtwaa fowadi huyo mwenye umri wa miaka 20 atalazimika kuweka mezani kima cha Sh21 bilioni.

Bellingham, 17, alirasimisha uhamisho wake hadi kambini mwa Borussia Dortmund mnamo Julai 2020 kwa kima cha Sh4.2 bilioni baada ya kuagana na Birmingham City.

Man-United waliwahi pia kumtuma kocha wao wa zamani Sir Alex Ferguson hadi uwanjani Deepdale kumtazama Bellingham akitandaza mpira uwanjani kabla ya kuwasilishia Birmingham ombi rasmi la kumsajili kiungo huyo muhula huu.

Ingawa hivyo, mafanikio ya hivi karibuni ya Dortmund katika kuwanoa vilivyo chipukizi Jadon Sancho, Christian Pulisic na Erling Braut Haaland, yalimchochea zaidi Bellingham kuingia katika sajili rasmi ya kikosi hicho cha Bundesliga ambacho pia kinafukuzia fursa ya kushiriki soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao.

Mnamo Agosti 2019, Bellingham alivunja rekodi ya mvamizi wa zamani wa timu ya taifa ya Uingereza, Trevor Francis kwa kuwa mchezaji mchanga zaidi kuwahi kuwajibishwa katika kikosi cha kwanza cha Birmingham akiwa na umri wa miaka 16 na siku 38 pekee.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Refa wa kike Stephanie Frappart azidi kuweka rekodi kwenye...

ODM, ANC kwenye mvutano wa ni nani ateuliwe naibu gavana...