• Nairobi
  • Last Updated December 8th, 2023 10:25 PM
Man-United wazamisha Chelsea 4-1 katika EPL ugani Old Trafford na kufuzu kwa soka ya UEFA 2023-24

Man-United wazamisha Chelsea 4-1 katika EPL ugani Old Trafford na kufuzu kwa soka ya UEFA 2023-24

Na MASHIRIKA

MANCHESTER United walijikatia tiketi ya kunogesha soka ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu ujao wa 2023-24 baada ya kukomoa Chelsea 4-1 katika mchuano wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) ugani Old Trafford, Alhamisi.

Carlos Casemiro aliwaweka wenyeji Man-United kifua mbele katika dakika ya sita kabla ya Anthony Martial kufunga bao la pili mwishoni mwa kipindi cha kwanza aliposhirikiana vilivyo na Jadon Sancho.

Nahodha Bruno Fernandes alipachika wavuni bao la tatu la Man-United kupitia mkwaju wa penalti baada ya kuchezewa visivyo na Wesley Fofana ndani ya kijisanduku katika dakika ya 78.

Kosa jingine la Fofana lilishuhudia Marcus Rashford akifunga bao la nne la Man-United kunako dakika ya 78 kabla ya Joao Felix kufuta machozi ya Chelsea dakika mbili kabla ya kipenga cha kuashiria mwisho wa mchezo kupulizwa.

Mechi hiyo ilikuwa ya nane kati ya 10 kwa Chelsea kupoteza chini ya kocha Frank Lampard. Baada ya kupoteza jumla ya michuano 16 kutokana na 37 ya hadi kufikia sasa msimu huu, Chelsea wanakamata nafasi ya 12 jedwalini kwa alama 43. Man-United ni wa tatu kwa pointi 72.

Ushindi wa Man-United ulihakikisha kwamba wanawapiku Liverpool ambao sasa watashiriki ligi ndogo ya Europa League katika soka ya bara Ulaya msimu ujao.

Ingawa hivyo, raha ya ushindi wa Man-United iliyeyushwa na jeraha baya la kipindi cha kwanza lililolazimisha winga matata raia wa Brazil, Antony dos Santos, akiondolewa uwanjani kwa machela. Nyota huyo aliumia alipokabiliana na Trevoh Chalobah na atakosa sasa fainali ya Kombe la FA itakayokutanisha Man-United na Man-City chini ya kipindi cha wiki mbili zijazo ugani Wembley.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Vyakula vinavyoweza kukupa ngozi inayong’aa

Serikali yakana madai kuwa wadukuzi wa Kichina waliingilia...

T L