• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 2:08 PM
Manchester City watandika Manchester United na kujizolea Kombe la FA

Manchester City watandika Manchester United na kujizolea Kombe la FA

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City waliweka hai matumaini ya kujizolea jumla ya mataji matatu msimu huu baada ya kukomoa majirani zao Manchester United 2-1 katika fainali ya 142 ya Kombe la FA iliyochezewa ugani Wembley, Uingereza.

Miamba hao walifaulu kuhifadhi ufalme wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) muhula huu baada ya kupiga Arsenal kumbo katika dakika za mwisho. Sasa wanapigiwa upatu wa kuangusha Inter Milan ya Italia kwenye fainali ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) itakayowakutanisha jijini Istanbul, Uturuki, mnamo Juni 10.

Mabao kutoka kwa Ilkay Gundogan katika dakika ya kwanza na 51 yalitosha kuvunia Man-City Kombe la FA kwa mara ya saba katika historia na kunyima Man-United fursa ya kutawazwa washindi wa taji hilo kongwe zaidi nchini Uingereza kwa mara ya 13. Man-United walifutiwa machozi na Bruno Fernandes aliyefunga penalti kunako dakika ya 33.

Miaka minne tangu wanyakue mataji matatu katika historia ya soka ya Uingereza (EPL, Kombe la FA na Carabao Cup), Man-City wanapania sasa kuwa kikosi cha kwanza baada ya Man-United mnamo 1998-99 kuwahi kutwaa EPL, Kombe la FA na UEFA katika msimu mmoja.

Taji la EPL waliloshinda msimu huu lilikuwa lao la tatu mfululizo na la tano katika kipindi cha misimu sita chini ya kocha Pep Guardiola ambaye pia amewahi kudhibiti mikoba ya Barcelona na Bayern Munich nchini Uhispania na Ujerumani mtawalia.

Guardiola aliteremsha dimbani kikosi chake cha kwanza ugani Wembley akiwa na kiu ya kuendea mabao ya haraka dhidi ya Man-United. Kichapo cha awali cha 1-0 kutoka kwa Brentford kilikomesha rekodi nzuri ya kutoshindwa kwao katika mechi 25 mfululizo za mashindano yote.

Fainali ya Juni 3, 2023 ilikuwa ya 12 kwa Man-City kunogesha kwenye Kombe la FA. Hadi walipojibwaga ulingoni, walikuwa wamepoteza fainali tano na kushinda sita za awali, ya karibuni zaidi ikiwa dhidi ya Watford waliokubali kichapo kinono cha 6-0 mnamo 2019.

Man City walitinga fainali ya Kombe la FA msimu huu baada ya kubandua Chelsea, Arsenal, Bristol City na Burnley katika hatua za mapema kabla ya kupepeta Sheffield United katika nusu-fainali. Hadi walipoteremka Wembley kuvaana na Man-United, hawakuwa wamefungwa bao katika mchuano wowote wa kipute hicho muhula huu.

Ni Preston North End pekee mnamo 1889 na Bury mnamo 1903 waliowahi kutia kapuni Kombe la FA bila kufungwa bao katika pambano lolote la kivumbi hicho.

Man-City wanaojivunia idadi kubwa zaidi ya mabao katika Kombe la FA msimu huu (19), wamekuwa na rekodi nzuri zaidi katika fainali za makombe ya soka ya Uingereza. Miamba hao sasa wametamalaki fainali sita tangu Guardiola aanze kudhibiti mikoba yao mnamo 2016. Hata hivyo, walikuwa wamepoteza fainali nne kati ya sita za awali ugani Wembley huku wakikosa kufunga bao mara tatu pekee.

Man-United walishuka ulingoni kwa fainali ya Juni 3, 2023 iliyokuwa yao ya 21 kwenye Kombe la FA wakiwa na kiu ya kuendeleza ubabe dhidi ya Man-City waliokubali kichapo cha 2-1 kutoka kwao katika EPL mnamo Januari 2023 ugani Old Trafford.

Walitarajiwa pia kuendeleza msururu wa matokeo bora baada ya kushinda mechi nne za mwisho katika EPL msimu huu na kufuzu kwa soka ya UEFA muhula ujao baada ya kuambulia nafasi ya tatu kwa alama 75 huku pengo la pointi 14 likitamalaki kati yao na Man-City.

Licha ya kuanza vibaya kampeni yao ya EPL msimu huu kwa vichapo kutoka kwa Brighton (2-1) na Brentford (4-0) walifunga muhula kwa matao ya juu kwa kuponda Chelsea 4-1 kisha kucharaza Fulham 2-1 ugani Old Trafford.

Mabingwa hao mara 20 wa EPL walikomesha ukame wa miaka sita wa mataji kabatini mwao msimu huu baada ya kocha Erik ten Hag kuwaongoza kutandika Newacastle United 2-0 ugani Wembley mnamo Februari na kutwaa Carabao Cup.

Fainali ya Juni 3, 2023 ilikuwa ya kwanza katika kipindi cha miaka mitano kwa Man-United kunogesha katika Kombe la FA. Walitinga hatua hiyo baada ya kung’oa Everton, Reading, West Ham United, Fulham na Brighton. Walishinda mechi nne za kwanza kwa mabao 3-1 kabla ya kudengua Brighton kwa penalti 7-6 baada y sare tasa kwenye nusu-fainali mnamo Aprili 23.

Mara ya mwisho kwa Man-United kutwaa Kombe la FA ni 2015-16 ambapo walihitaji muda wa ziada kulaza Crystal Palace 2-1. Hiyo ilikuwa miaka miwili kabla ya Chelsea kuwakung’uta 1-0 katika fainali nyingine ya kipute hicho.

Ni Arsenal pekee (mara 14) ambao wameshinda Kombe la FA mara nyingi zaidi kuliko Man United ambao wametawazwa mabingwa wa kipute hicho mara 12. Hata hivyo, Man-United ndio wamepoteza fainali nyingi zaidi ya kivumbi hicho (mara tisa).

Licha ya ufanisi wao dhidi ya Man-City katika EPL Januari, Man-United walikuwa wamepoteza mechi tatu kati ya nne za awali dhidi ya majirani zao hao kwa jumla ya mabao 12-4, kikiwemo kichapo cha 6-3 ligini mwanzoni mwa msimu huu.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mhubiri Paul Mackenzie awaambia wanahabari wamnunulie...

ADAK yapiga Wakenya 20 marufuku kwa kudaiwa kutumia dawa za...

T L