• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 7:55 PM
Manchester City yazamisha chombo cha Chelsea na kukaribia kileleni mwa jedwali la EPL

Manchester City yazamisha chombo cha Chelsea na kukaribia kileleni mwa jedwali la EPL

Na MASHIRIKA

MANCHESTER City walichupa hadi nafasi ya tano kwenye msimamo wa jedwali la Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) baada ya kucharaza Chelsea 3-1 uwanjani Stamford Bridge mnamo Jumapili.

Licha ya kukosa huduma za baadhi ya wanasoka wao wazoefu katika kikosi cha kwanza, Man-City ya kocha Pep Guardiola ilifunga wenyeji wao mabao matatu ya haraka chini ya dakika 16 za kipindi cha kwanza.

Man-City walifungua ukurasa wa mabao kupitia kiungo Ilkay Gundogan katika dakika ya 18 kabla ya chipukizi Phil Foden kupachika wavuni goli la pili dakika tatu baadaye. Goli hilo la Foden ambalo lilimwacha hoi kipa Edouard Mendy, lilichangiwa na kiungo matata raia wa Ubelgiji, Kevin de Bruyne.

Man-City walifungiwa bao lao la tatu kupitia De Bruyne aliyeshirikiana vilivyo na fowadi Raheem Sterling.

Machozi ya Chelsea ambao kwa sasa wanatiwa makali na kocha Frank Lampard yalifutwa na chipukizi Callum Hudson-Odoi aliyepokezwa krosi na Kai Havertz ambaye pia alimtatiza pakubwa kipa Zack Steffen aliyewajibishwa katikati ya michuma ya Man-City kwa sababu Ederson Moraes ambaye ni mlinda-lango chaguo la kwanza ana virusi vya corona.

Man-City kwa sasa wanajivunia alama 29 sawa na Tottenham Hotspur na Everton. Ni pengo la pointi nne pekee ndilo linalotamalaki kati ya Man-City na viongozi wa jedwali Manchester United na Liverpool.

Chelsea ambao wangepaa hadi kileleni mwa jedwali iwapo wangeshinda Everton mnamo Disemba 12, 2020, sasa wanashikilia nafasi ya nane jedwalini kwa alama 26 sawa na Aston Villa, West Ham United na Southampton ambao watakuwa wenyeji wa Liverpool mnamo Januari 4 uwanjani St Mary’s.

Mchuano huo ulikuwa wa kwanza kwa Man-City kusakata chini ya siku nane baada ya gozi la awali dhidi ya Everton mnamo Disemba 28 kuahirishwa kufuatia ripoti za maambukizi ya Covid-19 uwanjani Etihad.

Licha ya Man-City kukubaliwa kufungua uwanja wao wa mazoezi na kurejea kujiandaa kupepetana na Chelsea, kikosi hicho kilichotwaa ubingwa wa EPL mnamo 2017-18 na 2018-19, kilikosa maarifa ya wachezaji Kyle Walker, Gabriel Jesus, Ederson, Ferran Torres, Eric Garcia na Tommy Doyle.

Beki Benjamin Mendy aliyekiuka kanuni zinazodhibiti maambukizi ya Covid-19 nchini Uingereza baada ya kuandaa dhifa ya kuukaribisha mwaka mpya iliyohudhuriwa na wageni nyumbani mwake, alikuwa miongoni mwa wanasoka wanane waliopangwa kwenye kikosi cha akiba cha Man-City.

Mabao 13 ambayo Man-City muhula huu ndiyo idadi ndogo zaidi ya magoli ambayo kikosi chochote kimewahi kufungwa kufikia sasa kwenye EPL.

Chelsea walishuka dimbani kuvaana na Man-City wakitarajiwa kujinyanyua baada ya kujizolea alama nne pekee kutokana na mechi tano za awali ligini.

Chelsea kwa sasa wanajiandaa kualika Morecambe katika mechi ya raundi ya tatu ya Kombe la FA mnamo Januari 10 ugani Stamford Bridge kabla ya kuwaendea Fulham kwa minajili ya mechi ya EPL siku tano baadaye uwanjani Craven Cottage.

Kwa upande wao, Man-City watakuwa wageni wa Manchester United katika nusu-fainali ya Carabao Cup mnamo Januari 6 kabla ya kuwakaribisha Birmingham kwa mechi ya Kombe la FA Januari 10 uwanjani Etihad.

  • Tags

You can share this post!

Atletico Madrid wacharaza Alaves 2-1 na kurejea uongozini...

Kajiado All Stars wapepeta Kayole Youth na kutinga...