• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 10:55 AM
Manchester United wafuzu kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya

Manchester United wafuzu kucheza michuano ya Klabu Bingwa Ulaya

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

MANCHESTER United wanaweza kupumua sasa baada ya kubomoa Chelsea 4-1 mnamo Alhamisi na kujihakikishia nafasi katika Klabu Bingwa Ulaya msimu ujao.

Vijana wa kocha Erik ten Hag wamekuwa wakiangalia mgongoni mwao na kuhofia kufikiwa na Liverpool waliozoa ushindi mara saba mfululizo kabla ya kukabwa 1-1 na Aston Villa.

Katika kipindi hicho, United walizoa ushindi mara nne katika mechi saba kabla ya kuzima presha na matumaini ya Liverpool kwa kulima Chelsea.

Mashetani wekundu wa United walianza msimu na masaibu ya kupoteza mechi mbili za kwanza. Pia, supastaa Cristiano Ronaldo aligura klabu kabla ya United kuaibishwa 7-0 na Liverpool mwezi Machi.

Hata hivyo, Ten Hag anastahili sifa kwa kuongoza mabingwa hao wa zamani kumaliza ndani ya mduara wa nne-bora.

Hapo Alhamisi, United walipata mabao yao kupitia kwa Casemiro dakika ya sita, Anthony Martial (45+6), Bruno Fernandes (penalti dakika ya 73) na Marcus Rashford (78). Joao Felix alifungia Chelsea bao la kufuta machozi dakika ya 89.

Baada ya kichapo hicho cha 16 cha Chelsea mwaka 2023, kocha Frank Lampard alikiri kuwa tatizo kubwa msimu huu limekuwa kufunga mabao. Ameshinda mchuano mmoja kati ya 10 tangu ajaze nafasi ya Graham Potter.

Ten Hag alipongeza Casemiro kwa kazi nzuri na kuongeza kuwa United imepiga hatua muhimu kwa kufuzu kushiriki Klabu Bingwa inakostahili kuwa.

“Ni muhimu kumaliza katika mduara wa nne-bora. Klabu hii ni ya kiwango cha Klabu Bingwa. Si rahisi kupata tiketi katika Ligi Kuu ya Uingereza. Ni mashindano magumu yenye ushindani makali. Tumefuzu kwa hivyo msimu umekuwa mzuri,” alisema Mholanzi huyo.

Ushindi huo ulishuhudia United waking’oa Newcastle katika nafasi ya tatu.

Manchester City wanaongoza kwa pointi 89 wakifuatiwa na Arsenal (81), United (72), Newcastle (70) na Liverpool (66) katika nafasi tano za kwanza.

Ratiba ya Mei 28 (mechi zote 6.30pm):

Aston Villa v Brighton, Everton v Bournemouth, Leeds v Tottenham, Brentford v Manchester City, Manchester United v Fulham, Chelsea v Newcastle, Leicester v West Ham, Arsenal v Wolves, Southampton v Liverpool, Crystal Palace v Nottingham Forest.

  • Tags

You can share this post!

Nilikodishwa tu kusafirisha sukari, mshukiwa ajitetea

Ligi ya Saudi Arabia itakuwa tano-bora karibuni –...

T L