NA CHARLES ONGADI
BONDIA mwenye tambo kibao kutoka Tanzania, Karim ‘Mtu Kazi’ Mandonga ameratibiwa kuzichapa tena na Daniel Wanyonyi wa Kenya jijini Nairobi.
Mabondia hawa wamepangiwa kuchapana mnamo Julai 22 katika ukumbi wa Sarit Expo Centre baada ya kupigana mara ya kwanza Januari 14, 2023.
Katika pigano hilo, Mandonga alionyesha mbwembwe za kila aina akitumia ngumi aina ya ‘Sugunyo’ kumkomoa Wanyonyi, ambaye alisalimu amri raundi ya sita katika pambano hilo lililoratibiwa kuwa la raundi 10.
Aidha, Mandonga amerudi tena kutaka kuwadhihirishia mashabiki wake Afrika Mashariki na Kati kwamba yeye ndiye kidume katika uzito huo.
Kulingana na Afisa Mtendaji wa Ultra Fight Series Promotions, Maurice Odero, ambao ndio wadhamini kwa ushirikiano na Sarit Expo Centre, mabondia hawa wawili wameshatia sahihi mkataba wa shindano hilo litakaloandamana na mapigano mengine tisa.
“Nilimwacha Wanyonyi na jeraha la uso katika pigano letu la kwanza na nimerudi kumzika kabisa na kuthibitisha kuwa mimi ndiye kusema katika ngumi uzito wa Lightheavy hapa Afrika Mashariki,” akajigamba Mandonga.
Mandonga amefichua atatumia mtindo mpya unaofahamika kama ‘Kikuki’ kutokea nchini Urusi badala ya ule wa ‘Sugunyo‘ kutoka Ukraine aliotumia awali.
Hata hivyo, Wanyonyi amejitetea akisema kipindi akikutana na Mandonga mara ya kwanza alikuwa hajajifua vya kutosha lakini kwa sasa yuko fiti na ameahidi kupigana kinyama kumnyamazisha Mandonga.
“Wacha aje na staili zake zote kutoka Ukraine na Urusi lakini hapa lazima atalamba sakafu, nimerekebisha makosa ya awali na sasa niko poa kabisa,” akasema Wanyonyi ambaye ni bingwa wa zamani wa taji la Africa Boxing Union (ABU) alilonyakua mwaka wa 2014 baada ya kumkomoa Mkongomani Matamba Postolo kwao Kinshasa.
Mara ya mwisho mabondia hawa kupanda ulingoni ilikuwa ni Machi 25 katika ukumbi wa Moi International Sports Centre, Kasarani ambapo Mandonga aliimshinda Keneth Lukyamuzi wa Uganda na kunyanyua taji la Pugilistic Syndicate of Tanzania (PST) uzito wa Lightheavy.
Naye Wanyonyi akitumia dakika mbili pekee kumkomoa Charles Kakande pia wa Uganda kwa njia ya KO.