• Nairobi
  • Last Updated April 17th, 2024 7:55 PM
Maskini Homeboyz wajikwaa Ligi Kuu

Maskini Homeboyz wajikwaa Ligi Kuu

CECIL ODONGO na JOHN ASHIHUNDU

MATUMAINI ya Kakamega Homeboyz kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu kwa mara ya kwanza Jumapili yalipata pigo baada ya kupigwa 2-0 na AFC Leopards katika uga wa Bukhungu, Kaunti ya Kakamega.

Katika mechi nyingine, mabingwa wa zamani Gor Mahia waliokuwa na wachezaji 10 uwanjani walitoka nyuma na kuipiga Nairobi City Stars 3-2 katika uga wa MISC Kasarani .Ugani Ruaraka, FC Talanta iliipiga Kariobangi Sharks 2-0 nao Bidco United wakalemea Wazito 2-0 katika uga wa kitaifa wa Nyayo.

Katika mechi nyingine iliyosakatwa Magharibi ya nchi, Nzoia Sugar iliendelea kujizatiti kukwepa shoka la kushushwa ngazi baada ya kuibwaga KCB 1-0 katika uga wa Sudi, mjini Bungoma.

Ugani Bukhungu, Leopards ilichukua uongozi dakika ya nne katika kipindi cha kwanza kupitia kwa Collins Shivachi aliyefunga kwa kichwa kutokana na mpira wa ikabu wa Washington Munene.

Mshambuliaji raia wa Nigeria Ojo Olaniyi aliongeza bao la pili mnamo dakika ya 57 kupitia kwa shuti kali lililomshinda kipa wa Homeboyz Stephen Otieno.

Baada ya ushindi huo, Homeboyz sasa wana kibaru kigumu cha kutwaa ubingwa wa KPL kwa kuwa bado wanatoshana na Tusker kileleni kwa alama 57 japo inadunishwa na ubora wa mabao.

Homeboyz itacheza dhidi ya FC Talanta na Kariobangi Sharks huku Tusker ikipepetana na Bidco United na Posta Rangers katika mechi zake za kutamatisha ligi.

“Bado tuna nafasi ya kupigania taji la KPL katika mechi mbili zijazo. Ni kweli kuna wakati tuliongoza ligi kwa alama nyingi lakini katika soka haya mambo hutokea. Kuna mambo ya nje ya uwanja yaliyoathiri matokeo yetu lakini siwezi kuyazungumzia hadharani. Tutaendelea kutia bidii kuhakikisha tunashinda mechi zetu mbili zilizosalia,” akasema kocha wa Kakamega Homeboyz Bernard Mwalala.

Naye mwenzake wa AFC Leopards Patrick Aussems alisema kuwa ushindi huo ulidhihirisha ubabe wao katika debi ya Ingoo na kuwapa matumaini ya kumaliza miongoni mwa timu tano bora.

“Naamini sasa tuna uwezo wa kumaliza miongoni mwa timu tano bora. Japo walikuwa na presha wakipiania taji, tuliwadhibiti na mbinu zetu zilifanya kazi,” akasema Aussems.

Kwenye mechi ya Gor Mahia, bao la kujifunga la Dennis Wanjala kunako dakika ya 83 liliwapa KOgalo ushindi.

Timothy Ouma na Anthony Muki walifunga mabao ya City Stars huku Benson Omalla na Samuel Onyango pia wakicheka na nyavu za wapinzani wao kwa upande wa Gor Mahia.

  • Tags

You can share this post!

Chepng’etich ang’aria wapinzani mbio za 1500m Eugene...

Weta sasa kuvumisha Ruto kikamilifu akisubiri kutetea kiti...

T L