• Nairobi
  • Last Updated February 22nd, 2024 1:05 PM
Matano asema Tusker hawana mpango wa kumsajili Lewis Bandi wa AFC Leopards

Matano asema Tusker hawana mpango wa kumsajili Lewis Bandi wa AFC Leopards

NA JOHN ASHIHUNDU

KOCHA Robert Matano wa Tusker FC amesema klabu yake haina mpango wowote wa kumsajili Lewis Bandi anayeripotiwa kutoweka kwenye kambi ya AFC Leopards.

Matano alisema hayo kufuatia madai ya baadhi ya wafuasi wa Leopards kwamba staa huyo mwenye umri wa miaka 20 anafanya mazungmzo na mabingwa hao watetezi wa Ligi Kuu ya Kenya (FKF-PL).

Bandi alionekana mara ya mwisho wiki mbili zilizopita, Leopards ilipocheza na Kakamega Homeboyz kwenye nusu-fainali ya Mozzart Bet Cup na kushindwa kwa mabao 2-1.

Lakini akitetea klabu yake kuhusiana na uvumi huo, Matano alisisitiza kuwa habari hizo ni za uwongo.

“Sina mpango wowote wa kusajili mchezaji kutoka AFC Leopards,” alisema.

“Nimeshangaa kusikia habari hizi, wakati ambapo hata shughuli za usajili hazijaanza. Kuna watu mashuhuri ambao wamezoea kueneza uvumi kwa maslahi yao ya kibinafsi, na kamwe hawafai kuaminiwa. Siku chache zilizopita walisema tuna mpango wa kusajili mchezaji kutoka klabu moja ya Rwanda, lakini baadaye ikagunduliwa kuwa ulikuwa uwongo mtupu.”

Kwa upande mwingine, Leopards kupitia kwa mwenyekiti wake Dan Shikanda ilithibitisha kwamba Bandi ametoweka, na hajulikani aliko.

Hata hivyo, mwenyekiti huyo alisema kutokuwepo kwa mchezaji huyo hakuwapi wasiwasi wowote.

Shikanda alisema Leopards itakuwa na kikosi imara msimu ujao baada ya marufuku ya shirikisho la soka la FIFA kuondolewa na klabu sasa inaruhusiwa kusajili wachezaji wapya.

Bandi alikuwa mchezaji wa AFC Leopards Youth tangu 2015, kabla ya baadaye kupelekwa Hakati Sportiff ya Daraja la Pili kwa mkopo.

Alipanda bei baada ya kusajiliwa katika kikosi kikuu cha AFC Leopards mnamo 2020 akiwa na umri wa miaka 18.

Mwanafunzi huyo wa zamani ambaye anaweza kucheza katika sehemu tofauti kikosini alikuwa katika kikosi cha Chapa Dimba All Stars cha chipukizi waliozuru nchini Uhispania kwa ziara ya siku 10 kwa udhamini wa Safaricom.

  • Tags

You can share this post!

Sammy ‘Kempes’ Owino kuwania urais FKF

Makundi sasa kupata mkopo wa Hasla

T L