• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 10:55 AM
Mbio za Nyika za Pwani kufanyika Wundanyi Jumamosi

Mbio za Nyika za Pwani kufanyika Wundanyi Jumamosi

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

MWANARIADHA Mkenya aliye Marekani, Panuel Mkungo amewasili nchini kuiwakilisha timu ya nyumbani kwao ya Taita Taveta kwenye Mbio za Nyika za jimbo la Pwani zinazofanyika uwanja wa Dawnson Mwanyumba mjini Wundanyi hivi leo Jumamosi, Febuari 5.

Katika mbio hizo, timu ya Kaunti ya Taita Taveta itapigania kuhifadhi mataji yote manane yatakayoshindaniwa wakati wa mbio hizo zinazotayarishwa na kusimamiwa na tawi la jimbo la Pwasni la Chama cha Riadha cha Kenya (AK).

Mwenyekiti wa AK Pwani, Dammy Kisalu alisema kuwa mbio za mwaka huu zinatarajia kuwa na ushindani mkubwa kwani timu za Kilifi na Kwale zimefika huko Wundanyi mapema kwa ajili ya kuozea hali ya hewa iliyoko huko.

“Tuna imani kubwa mbio za mwaka huu zitakuwa na ushindani mkubwa kwani kaunti zote zimejiandaa vya kutosha huku wanariadha wake wakipigania kupata nafasi ya kuwa katika timu ya Pwani itakayoshiriki kwenye mbio za kitaifa,” akasema Kisalu.

Timu zitakazoshiriki ni zile za kaunti za Mombasa, Lamu, Kwale, Tana River, Kilifi na wenyeji Taita Taveta. Mwanariadha anayeishi Marekani, Panuel Mkungo amerudi nchini kuongoza kikosi cha Taita Taveta kuhifadhi mataji yake yote manane.

Mbio zitakazofanyika ni za kilomita 10 kwa wanaume na wanawake wakubwa, kilomita 6 kwa wasichana, kilomita 8 kwa wavulana, kilomita 5 kwa wasichana wa umri chini ya miaka 18 na kilomita 5 kwa wavulana wa umri chini ya miaka 18 na mbio za kupokezana vijiti ya mchanganyiko.

Majina mashuhuri ya wanariadha wenye majina makubwa wanaotarajiwa kushiriki ni Clara Nwazo na Lameck Mwakio wa Taita Taveta, Janet Sanita na Antonina Kenga (Kilifi).

Mbio za Nyika za kaunti sita za Pwani, Mombasa, Taita Taveta, Kwale, Kilifi, Tana River na Lamu zilifanyika Jumamosi iliyopita ambapo wanariadha bora walichaguliwa kuwakilisha kaunti zao kwenye mbio za leo za jimbo la Pwani.

You can share this post!

Buhari ateua mabalozi waliojiuzulu kuwa mabalozi

LAMU: Gavana Twaha ajiteua kuhudumu kama waziri