• Nairobi
  • Last Updated September 26th, 2023 10:25 PM
Mshambuliaji Rafael Leao sasa kuchezea AC Milan hadi mwaka wa 2028

Mshambuliaji Rafael Leao sasa kuchezea AC Milan hadi mwaka wa 2028

Na MASHIRIKA

FOWADI Rafael Leao, 23, ametia saini mkataba mpya wa miaka mitano utakaomdumisha kambini mwa AC Milan hadi mwaka wa 2028.

Sogora huyo raia wa Ureno amekuwa akihusishwa pakubwa na Chelsea ikizingatiwa kwamba kandarasi yake ya awali ugani San Siro ilikuwa ikatike rasmi mnamo 2024.

Leao alitua Milan mnamo 2019 baada ya kuagana na Lille ya Ufaransa.

Tangu wakati huo, amewajibishwa mara 162 na kufunga mabao 41 akichezea Milan ambao ni wafalme mara saba wa Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

Alitawazwa Mchezaji Bora wa Ligi Kuu ya Italia (Serie A) mnamo 2021-22 baada ya kusaidia Milan kunyanyua taji la kwanza la Serie A tangu 2011.

Leao amekuwa mhimili muhimu katika kikosi cha kocha Stefano Pioli msimu huu ambapo aliwaongoza kukamilisha kampeni za Serie A ndani ya mduara wa nne-bora na kutinga nusu-fainali za UEFA ambapo walibanduliwa na Inter Milan kwa jumla ya mabao 3-0.

Alikuwa pia sehemu ya kikosi cha Ureno kilichotinga robo-fainali za Kombe la Dunia nchini Qatar mnamo 2022.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Watu wawili wafariki kwenye ajali ya matatu na trekta Ndhiwa

Kigogo Sergio Ramos aagana rasmi na PSG

T L