NA TITUS OMINDE
BAADA ya miaka miwili ya kupigania kuachiliwa kwake kwa dhamana, Mahakama Kuu ya Eldoret mnamo Jumatano ilimwachilia huru Ibrahim Rotich anayekabiliwa na shtaka la mauaji ya mkewe Agnes Tirop ambaye alikuwa mwanariadha wa kimataifa.
Rotich ameachiliwa kwa dhamana ya Sh500,000 pesa taslimu au dhamana ya Sh400,000 na mdhamini sawa.
Akitoa uamuzi wake, Hakimu Robert Wananda Anuro aliamuru mshtakiwa aachiliwe kwa dhamana baada ya ripoti ya maafisa wa kurekebisha tabia kumpendelea.
Rotich anashtakiwa kwa kumuua mkewe ambaye walikuwa wameachana.
Kabla ya kifo chake, Tirop alikuwa bingwa wa zamani wa mbio za nyika.
Aliuawa katika nyumba yao mjini Iten mnamo Oktoba 13, 2021.
Mshukiwa anadaiwa kumuua kufuatia ugomvi wa kinyumbani uliozuka usiku huo wa maafa.
Alipofika kortini kwa mara ya kwanza, alikana shtaka hilo mbele ya jaji Reuben Nyakundi.
Jaji Anuro alisema hakukuwa na sababu za msingi za kuendelea kumshikilia mshtakiwa rumande kwa kuwa mazingira yaliyoilazimu mahakama kumnyima uhuru tayari yamebadilika.
“Kwa miaka miwili iliyopita mshitakiwa amekuwa akizuiliwa rumande akihusishwa na mauaji ya mkewe, uamuzi huu unaambatana na tabia yake na mazingira ya nje ya gereza endapo ataachiwa,” akaamua Jaji Anuro alipomwachilia Bw Rotich.
Jaji Anuro alitoa maagizo kadhaa ambayo mshtakiwa anapaswa kuzingatia kufuatia kuachiliwa kwake kwa dhamana.
Mahakama ilionya kuwa endapo mshtakiwa atashindwa kutimiza matakwa ya awali, dhamana yake itafutiliwa mbali.
Miongoni mwa masharti ambayo mahakama ilimpa ni pamoja na kuripoti katika afisi za DCI mjini Eldoret kila Jumatatu.
Hata hivyo mahakama ilitoa masharti makali dhidi ya mshtakiwa ili kuona kwamba bondi yake hatupiliwi mbali.
Mahakama ilimwonywa dhidi ya kutembelea au kushirikiana na familia ya marehemu katika mazungumzo bila idhini ya mahakama, pamoja na mashahidi kuepusha kuingilia mashahidi wa upande wa mashtaka.
Mahakama pia ilimuagiza asizuru nyumba yake ya mjini Iten katika Kaunti ya Elgeyo Marakwet ambayo ingali inachukuliwa kuwa eneo la uhalifu.
Vile vile amezuiwa kusafiri nje ya kaunti yake ya Uasin Gishu asipokuwa na kibali kutoka kwa makachero wa DCI.
“Hupaswi kutengamana na mashahidi wa serikali ukikwenda kinyume na masharti haya yote, dhamana yako itafutiliwa mbali mara moja,” alionya Jaji Anuro.
Aidha Jaji Anuro alimwamuru Bw Rotich kukabidhi hati yake ya kusafiria kwa mahakama au DCI kwa hifadhi salama hadi kusikizwa na kuamuliwa kwa kesi dhiid yake.
Kesi hiyo itaendelea kusikilizwa wiki hii.