• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 9:55 AM
Mwanariadha mkimbizi Mkongo aliyekimbia kutoka Nairobi hadi Mombasa apokelewa kishujaa

Mwanariadha mkimbizi Mkongo aliyekimbia kutoka Nairobi hadi Mombasa apokelewa kishujaa

Na GEOFFREY ANENE

MKIMBIAJI mkimbizi Francois Msafiri amepokea mapokezi ya kishujaa mtaani mwake Syokimau baada ya kukamilisha mbio za zaidi ya kilomita 500 kutoka Nairobi hadi Mombasa kati ya Juni 4 na Juni 6.

Makumi ya bodaboda walifurika katika barabara ya Sykimau-Katani Road kusherehekea mafanikio hayo ya kipekee ya raia huyo wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.

Walipiga honi na kufurahia ushindi huo wa aina yake wa Msafari ambaye alikuwa amejitokeza dirishani katika gari moja ndogo jeusi kusherehekea.

“Nashukuru kunipokea nyumbani. Najivunia kufika nyumbani kutoka Mombasa. Nilishiriki mbio kutoka Nairobi hadi Mombasa ili kuhamasisha Wakenya umuhimu wa kusaidia watoto wakimbizi humu nchini kupata elimu bora,” alisema mkimbiaji huyo.

Katika mahojiano alipofika mjini Mombasa mnamo Jumapili, Msafiri alisisitiza kuwa anatumia riadha kuchangisha fedha za kuimarisha elimu ya watoto wanaoishi katika kambi za wakimbizi.

“Nashiriki mbio hizi ili kuchangishia watoto fedha kuwawezesha kukamilisha masomo yao. Wengi wao wanapata mimba za mapema, wengine wameingilia dawa za kulevya na ninataka kubadilisha mkondo huo mbaya,” alisema Msafiri.

Alifichua kuwa alitumai kukamilisha umbali huo akitumia saa 40, lakini haikuwezekana kwa sababu alichanika msuli kidogo baada ya kilomita ya 300.Meneja wake na kocha Enock Rotich alisema kuwa alifurahia kuwa walifaulu kufika Mombasa.

“Tunafurahi kufika Mombasa baada ya safari ndefu na ya kuchosha. Pongezi kwake. Tunachangisha fedha kusaidia watoto wakimbikizi kielimu na pia kukuza talanta zao. Imekuwa safari ndefu. Tunashukuru maafisa wa usalama katika barabara tuliyotumia kwa kutuelewa licha ya kuwa tuliendelea na safari hata wakati wa kafyu,” alisema Rotich.

Changamoto kubwa, alisema, ilikuwa malori makubwa barabarani yaliyosababisha wapoteze muda.

Katibu wa Shirikisho la Riadha Kenya kaunti ya Mombasa, Beatrice Taita alipongeza mwanariadha huyo na kuomba kaunti hiyo itoe mchango wake pamoja na kujenga kambi ya wakimbizi kushughulikia masuala yao.

Afisa anayesimamia michezo katika kaunti ya Mombasa, Innocent Mugabe, aliahidi kuwa kaunti itasaidia kampeni yake na kupongeza juhudi zake za kusaidia watoto.

You can share this post!

Raila atetea miradi ya handisheki

Kevin de Bruyne ajumuika na wenzake kambini mwa Ubelgiji...