• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
Nairobi Water Queens balaa katika Handiboli nchini

Nairobi Water Queens balaa katika Handiboli nchini

Na JOHN KIMWERE

TIMU ya kina dada ya Nairobi Water Queens imeonesha handiboli ya kuvutia hapa nchini kwenye kampeni za Ligi Kuu ndani ya misimu nane sasa.

Aidha warembo hao wameibuka moto wa kuotea bali kwenye mechi za kuwania kombe la Klabu Bingwa Afrika Mashariki na Kati (ECAHF).  Nairobi Water Queens ya kocha, Jack Ochieng imehifadhi taji la Ligi Kuu kwa mara ya nane mfululizo baada ya kumaliza kileleni mwa jedwali kwenye mechi za kipute hicho muhula uliyomaliza wiki iliyopita.

Vipusa hao chini ya na Gladys Chillo walihitaji hilo baada ya kumaliza mechi zao bila kushindwa wala kudondosha alama hata moja.

KUTAWALA

Wasichana hao wanaolenga kutawala katika mchezo huo barani Afrika endapo watapata udhamini walishinda mechi zote 14 ambapo waliibuka kifua mbele kwa kuzoa pointi 28, nne mbele ya Ulinzi Sharks. Nao malkia wa zamani, Halmashauri ya Nafaka na Mazao nchini (NCPB) waliridhika na nafasi ya tatu kwa alama 18, moja mbele Nanyuki Ladies.

Kwenye patashika ya kukunja jamvi, Nairobi Water ilinyuka Nanyuki Ladies kwa mabao 31-19 uwanjani Nyayo Stadium, Nairobi. Cecilia Katheu na Brenda Ariviza waliibuka wafungaji bora upande wa Nairobi Queens walipocheka na nyavu mara sita na tano mtawalia. Marsore Okwakau alionyesha uhodari wake alipofungia Nanyuki Ladies mabao 11.

Timu ya Nairobi Water Queens ya mchezo wa handiboli…Picha/JOHN KIMWERE

”Katika mpango mzima ninashukuru wachezaji wangu kwa kukaza buti na kufaulu kuhifadhi kombe hilo. Hakika hatukushinda taji hilo kiulaini bali bidii yetu imechangia pakubwa kuibuka mabingwa tena,” kocha huyo alisema na kuongeza licha ya kukosa ufadhili wa kutosha hakuna kuvumua wataendelea kujituma kadiri ya uwezo.

Kina dada hao waliandikisha rekodi nyingine walipohifadhi taji la ECAHF kwa mara ya saba mfululizo mwezi uliyopita kwenye mechi zilizoandaliwa Dar es Salaam, Tanzania. Kocha wa Malkia hao anazidi kushikilia kuwa timu za Kenya bado zinahitaji kushiriki mechi nyingi za kupimana nguvu dhidi ya wenzao kutoka mataifa mengine Afrika maana vikosi nyingi katika ukanda ya Afrika Mashariki havina uzoefu wa migarazano ya kimataifa.

MAPENDELEO

Hata hivyo kocha huyo na kamati yake ya kiufundi wanashangaa pakubwa maana licha ya kubeba taji hilo mara saba hakuna msimu wowote timu hiyo iliyowahi kuteuliwa kuwania tuzo ya timu bora ya mwaka. ”Kiukweli hatuna budi kutaja kuwa kwenye tuzo za SOYA huwa na mapendeleo maana hatuelewi ni mtindo gani hutumika kwa timu kuteuliwa kuwania tuzo hizo,” alidokeza na kuongeza wahusika wakome kubagua fani zingine.

Kando na michuano hiyo warembo hao kabla ya mechi za msimu mpya kukunjua jamvi watashiriki ngarambe ya kutetea kombe waliloshinda muhula uliyopita la Super Cup. Kikosi hicho kinashirikisha wachezaji kama:Eunice Oginga na Modesta Auma (golikipa). Winga:Glady’s Chilo, Faith Mukhala, Jane Waithera, Cecilia Katheu,

na Mercy Katola. Safu ya Kati: Tracy Awino, Rose Ambongo, Mercy , Lucy Auma, Melvin Akinyi, Michele Adhiambo na Brenda Musambai.

SAFU YA NYUMA; Brenda Ariviza, Elizabeth Kemei na Vallarie Adhiambo.

Kamati ya Kiufundi: Jack Habert, Thodosia Sangoro na Caroline Kusa.

Timu ya Nairobi Water Queens ya mchezo wa handiboli…Picha/JOHN KIMWERE

You can share this post!

Waya ya stima yakatiza uraibu wa kozimeni aliyetesa wenyeji

Mchezaji wa zamani wa Gor atua Somali

T L