• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:37 AM
Nanjala kupiga jeki maandalizi ya Harambee Starlets gozi la WAFCON licha ya tetemeko kumuathiri kisaikolojia

Nanjala kupiga jeki maandalizi ya Harambee Starlets gozi la WAFCON licha ya tetemeko kumuathiri kisaikolojia

NA TOTO AREGE

MSHAMBULIZI matata wa Harambee Starlets Violet Nanjala anatarajiwa kuingia kambini Ijumaa wiki hii, kwa maandalizi ya mechi za mchujo wa kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) 2024.

Tayari wachezaji 17 kati ya 30 walioitwa kambini na kocha Beldine Odemba, wameanza mazoezi katika uwanja wa Kasarani Annex jijini Nairobi. Starlets watamenyana na Indomitable Lionesses ya Cameroon.

Tetemeko la ardhi la hivi majuzi huko Marrakech, Morocco anakochezea Nanjala, limemuathiri kisaikolojia.

Nanjala, 21, anachezea Klabu ya Club Municipal de Laayoune katika Ligi ya Wanawake na Morocco na anaishi Laayoune, ambako ni umbali wa kilomita 864.7 kutoka Marrakech. Hakujua chochote kilochotokea usiku wa kuamkia Jumamosi.

“Kwa kuwa sizungumzi Kiarabu kwa ufasaha, lugha inayozungumzwa nchini Morocco, niliwatafuta wachezaji wenzangu klabuni kuelewa kilichotokea. Mmoja wao, ambaye anafahamu Kiarabu na Kiingereza, alielezea matukio ya usiku uliopita. Nina hofu kubwa sana kwa kuwa vifo vinaongezeka kila kukicha,” alisema Nanjala.

Wachezaji ambao wamewasili kambini ni pamoja na mabeki wa Kenya Police Bullets Lavender Atieno Okeyo, Quinter Owiti, Valentine Kwaka na Puren Alukwe (kiungo).

Beki Phoebe Owiti na kiungo Janet Moraa Bundi wa Vihiga Queens na Airine Madalina (Bunyore Starlets) ni miongoni mwa wachezaji wa ndani. walio kambini.

Corazone Aquino (kiungo), Topister Situma (mshambulizi), Carolyne Rufa (kipa), Ruth Ingotsi (beki) na Elizabeth Wambui (kiungo) pia wameripoti kambini.

Mabeki wengine wa kigeni waliopo kambini ni; Lavender Okeyo, Quinter Owiti, Dorcas Shikobe, Christine Awour. Kipa Annedy Kundu na kiungo Mercyline Anyango pia wako kambini.

Hatua ya kwanza ya raundi ya kufuzu imepangwa kufanyika Septemba 22, 2023, na mkondo wa pili utafanyika nyumbani Septemba 26, 2023.

Hii itakuwa mechi ya kwanza ya kimataifa kwa Starlets tangu Kenya kuanza tena soka la kimataifa, kufuatia kuondolewa marufuku iliyowekwa na Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) kutokana na kuingiliwa na serikali mwezi Novemba mwaka 2021.

  • Tags

You can share this post!

Mabilioni yasubiri watu binafsi serikali ikifungua milango...

Hospitali Eldoret yashangazwa na idadi kubwa ya vijana...

T L