• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 11:30 AM
Ni kufa kupona Harambee Starlets wakishuka dimbani dhidi ya wenyeji Botswana

Ni kufa kupona Harambee Starlets wakishuka dimbani dhidi ya wenyeji Botswana

NA TOTO AREGE

KIVUMBI kikali kinatarajiwa jijini Gaborone nchini Botswana mnamo Jumanne, wakati The Mares ya Botswana itatifuana na Harambee Starlets ya Kenya katika mechi ya marudiano ya kufuzu Kombe la Wanawake la Mataifa ya Afrika (WAFCON).

Mechi hiyo itachezwa katika uwanja wa Taifa wa Gaborone nchini Botswana, kuanzia saa kumi jioni. Mshindi wa jumla atafuzu moja kwa moja kucheza WAFCON nchini Morocco mwakani.

Timu hizi mbili zilitoka sare ya 1-1 katika mechi ya kwanza katika uwanja wa Kitaifa wa Nyayo jijini Nairobi Jumatano iliyopita.

Mshambulizi wa Botswana Keitumtse Dithebe alifunga bao la kwanza katika dakika ya 38 kabla ya kiungo Marjolene Nekesa kusawazisha katika dakika ya 48.

Starlets itahitaji kushinda 2-0 au  sare ya mabao mengi ili kufuzu kwa Wafcon.

Kenya chini ya kocha Beldine Odemba inatafuta kurejea WAFCON tangu mwaka 2016, waliposhindwa kusonga mbele kutoka hatua ya makundi wakipoteza 3-1, 4-0 na 3-1 dhidi ya Ghana, Nigeria na Mali mtawalia.

Starlets walifika Botswana Jumapili na kufanya mazoezi siku  hiyo hiyo katika Uwanja wa Lekidi Football Center huko Gaborone.

Kuelekea mchezo huo, timu hizo mbili zimekutana mara mbili katika historia, na pambanao lao la mwisho lilikuwa mwaka 2015 wakati wa michuano ya kufuzu kwa Olimpiki. Kenya ilipoteza 2-1 Botswana katika mchezo wa kwanza na kushinda 1-0 nyumbani katika mchezo wa pili, hatimaye kufuzu kwa raundi iliyofuata kwa jumla ya mabao 2-2 kwa faida ya mabao ya ugenini.

Kufuzu kwa raundi ya pili ya kufuzu WAFCON, Starlets iliiondoa Indomitable Lionesses ya kwa mikwaju ya penalti ambapo Kenya ilishinda 4-3.

Mechi hiyo ilimalizika kwa sare ya 1-1 muda wa kawaida, na kusababisha mikwaju ya penalti.

Botswana kwa upande mwingine iliifunga Gabon  jumla ya mabao 7-1. Kwa ushindi wa 3-0 na 4-1 ugenini.

Akiongea Jumatatu katika mkutano na waandishi wa habari nchini Gaborone, Odemba alisema kuwa timu iko na morali kupata ushindi mbali na nyumbani.

“Sina wasiwasi wa majeruhi katika timu yangu kwani kila mchezaji atakuwa tayari kuchaguliwa. Tutawashinikiza wasichana wacheze vizuri. Tungojee mchezo wetu Jumatano,” alisema Odemba.

“Timu ya Botswana imefanya maandalizi ya kutosha na ina ufahamu kamili kuhusu wapinzani wetu kwa kuelewa uwezo wa kila mchezaji. Wana kikosi chenye uzoefu zaidi, wachezaji 11 ambao walianza katika mechi ya kwanza wanacheza soka la kulipwa. Kwa upande wetu, wachezaji wanne pekee wanacheza nje ya nchi na hii ni idadi ndogo,” alisema kocha wa Botswana Alex Malete.

Hii itakuwa mechi kubwa kwa Starlets kwani Botswana wana faida ya bao la ugenini na pia uwepo wa mashabiki wa nyumbani.

Botswana nao watakuwa wanajaribu kuzuia waliyofanya Kenya, ili kujaribu kupata droo ya 0-0 kwa dakika 90 na hivyo kuwapeleka moja kwa moja WAFCON.

Kenya inajilaumu kwa kutopata alama tatu nyumbani, baada ya nguvu mpya Violet Nanjala kupoteza penalti katika dakika za lala salama kipindi cha pili.

Kipa wa Harambee Starlets Annedy Kundu (katikati) akiwa mazoezini na makipa wengine mnamo Jumapili katika Uwanja wa Lekidi Football Centre jijini Gaborone, Botswana, kabla ya mechi yao ya kurudi dhidi ya The Mares ya Botswana, katika mechi ya kufuzu kwa Kombe la Mataifa ya Afrika kwa Wanawake (WAFCON) mwaka 2024. PICHA | HISANI | FKF
  • Tags

You can share this post!

Taasisi 70 za kozi za kiufundi kupigwa jeki ya Sh8.8 bilioni

Muchai aliuawa na jambazi sugu chini ya dakika moja,...

T L