• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 6:55 PM
Njia ya Gaspo Women kuendea ubingwa KWPL yageuka telezi

Njia ya Gaspo Women kuendea ubingwa KWPL yageuka telezi

NA AREGE RUTH

GASPO Women wamekosa nafasi ya kurejesha uongozi wao katika Ligi Kuu ya Wanawake nchini (KWPL), baada ya kutoka sare ya 1-1 na Ulinzi Starlets katika uwanja wa GEMS Cambridge mnamo Alhamisi.

Huku mechi mbili mbili zikiwa zimesalia kukamilika kwa msimu wa 2022/23, Vihiga Queens wanaongoza jedwali kwa pointi 49 katika mechi 20 kufuatia ushindi wa 3-0 dhidi ya Wadadia Women uwanjani Moi jijini Kisumu wikendi iliyopita.

Baada ya sare hiyo, Gaspo iko katika nafasi ya pili kwa alama 47, Ulinzi ni ya tatu kwa alama 39.

Kiungo Lydia Waganda aliiweka Gaspo mbele dakika ya 30, baada ya kuunganisha krosi ya kiungo Elizabeth Wambui na kuwafanya waongoze katika kipindi cha kwanza.

Kipindi cha pili, Gaspo iliyefanya mabadiliko ya kuongeza kasi ya mashambulizi lakini mabadiliko hayo hayakufua dafu.

Mshambulizi Layvne Achola aliingia badala ya Ann Nabwire dakika ya 63 huku Emily Okute akimpisha Lydia Akoth dakika ya 81.

Kiungo Elizabeth Wambui alipata jeraha dakika 88 na nafasi yake ikachukuliwa na Josephine Nana.

Dakika ya 87, Gaspo angeweza kuongeza bao la pili kupitia kwa Diana Wacera kupitia mpira wa kichwa kutoka kona, lakini beki wa Ulinzi Mary Ojenge alikuwa imara kazini.

Mshambulizi wa Ulinzi, Fasila Adhiambo alipata nafasi mbili za wazi dakika ya 50 na 60 kutokana na shambulizi la kaunta, lakini mabeki wa Gaspo akijumuisha Nuru Hadima na Leah Andiema walikuwa imara kwenye safu ya ulinzi.

Dakika za lala salama za kipindi cha pili, Ulinzi walipata penalti baada ya mshambulizi Joy KingLady kuangushwa kwenye eneo la hatari na beki wa Gaspo, Nuru Hadima. Denda Mary Ojenge alifunga bao la kusawazisha kutoka kwa mkwaju huo.

Kocha wa Ulinzi Joseph Mwanzia, alifurahishwa na sare hiyo akisema ilikuwa motisha kubwa kuelekea nusu fainali ya kombe la FKF la Wanawake wikendi ijayo.

“Walitufunga katika mkondo wa kwanza, tulilazimika kuhakikisha tunalipiza kisasi. Nataka niwashukuru washambulizi wangu waliojitoa leo. Kwa upande mwingine mlinda mlango wa mpinzani wetu Valentine Khwaka alifanya kazi nzuri kwa aliokoa nafasi nyingi,” amesema Mwanza.

Mkufunzi wa makipa wa Gaspo James Ombeng, amemlaumu mwamuzi wa kati kwa uchezeshaji mbaya.

“Tulicheza vizuri leo lakini mwamuzi alizembea kazini. Alitunyima penalti ya wazi lakini naweza kutoa hakikisho kuwa tuko kwenye mbio za ubingwa, tutapambana hadi mwisho,” amesema Ombeng’.

Mechi kati ya Kisumu All Starlets na Kayole Starlets iliyokuwa imeratibiwa kuchezwa katika uwanja wa Moi jijini Kisumu, haikuchezwa baada ya Kayole kukosa kujitokeza kucheza. Kisumu imepewa pointi tatu na mabao mawili.

Trans Nzoia Falcons wametawala nyumbani, walipoilaza Nakuru City Queens 3-2 katika uwanja wa Ndura mjini Kitale.

Mabao ya Falcons yamefungwa na Felistus Erima, Jekemoi Judy na Linda Kihara katika dakika ya 23, 28 na 52 mtawalia.

Mshambulizi Elizabeth Muteshi amefungia Nakuru mabao mawili dakika ya 45, 68 na kumfanya afikishe mabao 12 msimu huu.

Katika mechi nyingine katika Shule ya Upili ya Wavulana ya Dagoretti jijini Nairobi, mabingwa watetezi Thika Queens waliwapa walinyeshea Kangemil Ladies 8-1.

Mshambulizi Wendy Atieno, ambaye amekuwa nje akiuguza jeraha la pua, alifunga mabao manne katika dakika za 26, 58, 65 na 82 mtawalia. Sasa ndiye mfungaji bora wa ligi akiwa na mabao 17 sawa na mshambuliaji wa Bunyore Starlets Airin Madalina.

Linda Atwang amefunga mabao mengine dakika ya 48, 54, 71 na 79.

Consolata Oketch amefunga bao pekee la Kangemi dakika ya 86.

  • Tags

You can share this post!

Idadi ya waliothibitishwa kufariki Shakahola yagonga 235

Shakahola: Awamu ya pili ya upasuaji maiti kuanza Mei 24

T L