• Nairobi
  • Last Updated December 5th, 2023 8:55 PM
NYOTA WA WIKI: David Raya

NYOTA WA WIKI: David Raya

NA GEOFFREY ANENE

DAVID Raya Martin ni mmoja wa makipa wanaofanya vyema kwenye Ligi Kuu ya Uingereza.

Mhispania huyo anayeaminika kuwa mbioni kuhamia klabu kubwa kutoka Brentford, alianzia kucheza soka ya watu wazima katika klabu ya Blackburn Rovers na kisha akajiunga na Brentford katika Ligi ya Daraja la Pili mwaka 2019.

Alichangia pakubwa katika Brentford kupandishwa ngazi hadi Ligi Kuu mwaka 2021.

Kabla ya kuingia Uingereza, Raya alisakata soka ya wachezaji watano kila upande (futsal) na kisha talanta yake kupaliliwa na klabu ya UE Cornella.

Alipata udhamini wa kuendeleza kipaji chake kutoka kwa Blackburn Rovers mnamo Julai 2012.

Raya alisaini kandarasi ya kwanza ya soka ya malipo Februari 26, 2014 na kupata kucheza soka ya watu wazima kwa mara ya kwanza akiwa Southport kwa mkopo kutoka Blackburn Rovers msimu 2014-2015. Aliichezea mara 24.

Aliporejea ugani Ewood Park, alisaini kandarasi mpya ya miaka mitatu mnamo Aprili 2015.

Alikuwa kipa nambari mbili nyuma ya Jason Steele kabla ya kuwa nambari moja msimu 2016-2017. Alikuwa michumani mara 47 msimu 2017-2018 klabu hiyo ikiingia Ligi ya Daraja ya Pili. Alihifadhi nafasi yake 2018-2019 akicheza 46.

Raya aliondoka Rovers mnamo Julai 6, 2019 baada ya kuichezea mara 108 na kujiunga na Brentford kwa kandarasi ya miaka minne.

Uchezaji wake katika nusu ya kwanza ya msimu 2019-2020 ulishuhudia akijumuishwa katika orodha ya wawaniaji wa kipa bora wa mwaka wa tuzo za London Football mwaka 2020. Hakufungwa bao katika mechi 16 msimu huo.

Raya alikuwa katika kikosi cha Brentford kilichokosa pembamba kuingia Ligi Kuu msimu 2020-2021 baada ya kupoteza dhidi ya Fulham 2-1 katika awamu ya muondoano.

Aliachwa nje ya kikosi la mechi za kujiandaa kwa msimu 2020-2021 na michuano kadhaa ya kwanza ya mashindano akiuguza jeraha na pia kuhusishwa na uhamisho.

Hata hivyo, alirejea kikosini na kusaini kandarasi ya miaka minne mnamo Oktoba 2, 2020.

Raya ameng’ara michumani mwa Brentford tangu wakati huo akivutia klabu kadhaa kubwa zikiwemo Arsenal, Manchester United na Tottenham Hotspur.

Kimataifa, Raya alianza kuchezea Uhispania mwezi Machi 2022 katika mechi za kirafiki.

Alikosa kampeni yote ya Uhispania kwenye Ligi ya Mataifa ya Ulaya msimu 2022-2023. Alikuwa katika kikosi kilichoshiriki Kombe la Dunia nchini Qatar mwaka 2022, ingawa hakutumika.

  • Tags

You can share this post!

Azimio wakemea kiongozi wa mashtaka ICC

Siasa za upinzani si fani yangu – Sabina

T L