• Nairobi
  • Last Updated May 21st, 2024 8:55 PM
NYOTA WA WIKI: Kaoru Mitoma

NYOTA WA WIKI: Kaoru Mitoma

NA GEOFFREY ANENE

JE, Kaoru Mitoma anaweza kuwafikia Thierry Henry, Neymar na Eden Hazard kimchezo?

Ndilo swali ambalo wengi wanajiuliza baada ya winga huyo kutoka Japan kusakata soka safi kiasi cha kulinganishwa na masupastaa hao.

Mchawi huyo wa kuchenga anachezea Brighton & Hove Albion kwenye Ligi Kuu ya Uingereza (EPL). Anatumia mguu wa kulia.

Ametumiwa na Brighton na Japan katika wingi ya kushoto ambako anahangaisha wapinzani na chenga zake kali.

Mitoma aliwahi kucheza dhidi ya nahodha wa Harambee Stars Michael Olunga kwenye Ligi Kuu ya Japan wakiwa Kawasaki Frontale na Kashiwa Reysol mtawalia.

Walikutana Desemba 19, 2020, wakati Olunga na Yusuke Segawa walifungia Reysol bao moja kila mmoja katika kipindi cha kwanza.

Kisha Kawasaki wakapata ushindi baada ya kutinga magoli matatu kupitia kwa Akihiro Ienaga (mawili) na Leandro Damiao kipindi cha pili.

Mitoma alisuka pasi mbili za mwisho zilizozalisha mabao.

Alichezea Kawasaki jumla ya mechi 62 akijaza kimiani magoli 30 na kumega pasi 20 za mwisho zilizoishia kufungwa.

Kisha, alinyakuliwa na Brighton mnamo Agosti 10, 2021 kwa kandarasi itakayokatika Juni 30, 2025.

Hakuchezea Brighton katika msimu wa kwanza wa 2021-2022 kutokana na matatizo ya kupata kibali cha kucheza Uingereza.

Badala yake, Brighton ilimpeleka Union Saint-Gilloise kwa mkopo alikopata uzoefu.

Alichangia mabao manane na pasi nne zilizozalisha mabao katika michuano 29 huku klabu hiyo ikikamilisha msimu wa kawaida juu ya jedwali.

Ameingia EPL msimu huu wa 2022-2023 baada ya kupata kibali na kudhihirisha ana talanta ya ajabu.

Mitoma amefuma wavuni mabao sita na kumegea wachezaji wenzake pasi mbili zilizofungwa. Yeye ni mbunifu.

Si mchoyo katika kupasia wachezaji wenza mpira.

Mitoma, 25, amefunga mabao kadhaa matamu yanayoweza kuwania kuwa goli bora la msimu.

Kimataifa, Mitoma amechezea Japan mara 13 ikiwemo kwenye Olimpiki 2021 mjini Tokyo na Kombe la Dunia 2022.

  • Tags

You can share this post!

MALENGA WA WIKI: Nyakundi ni mshairi na mhariri wa riwaya,...

Benki ya CIB yasifu Kenya kwa ustawi wa upesi kidijitali

T L