• Nairobi
  • Last Updated December 4th, 2023 7:22 PM
Pinecrest Academy mabingwa wa karate kanda ya Mlima Kenya

Pinecrest Academy mabingwa wa karate kanda ya Mlima Kenya

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE ya Msingi ya Pinecrest Academy ya Juja ndio mabingwa wa Ligi ya Karate ya Shule za Kanda ya Mlima Kenya.

Kwenye michuano iliyoandaliwa katika ukumbi wa Pastoral Centre mjini Thika, mwishoni mwa wiki jana, wanakarate hao chipukizi waliongoza katika kategoria ya shule za msingi nane zilizoshiriki.

Kocha Lee Ng’ang’a anayejivunia mshipi wa 2nd Dan alisema vijana wake wote 14 walizoa medali tofauti kwenye mashindano hayo.

Kulingana na kocha huyo, vijana watatu waliibuka na medali ya dhahabu, wengine watatu wakazoa medali ya fedha, huku wanane wakijivunia shaba.

“Wanakarate hao ni wa uri wa kati ya miaka mitano na 10. Wote wamejitolea mhanga kucheza karate bila kurudi nyuma,” alisema kocha huyo.

Alisema amenoa kikosi hicho kwa chini ya miaka miwili pekee jambo alilosema ni la kujivunia.

Meneja mkuu wa shule hiyo Grace Macharia alikiri kuwa ushirikiano wa karibu baina ya kocha huyo na wazazi umezaa matunda.

Baadhi ya wachezaji wa Pinecrest Academy na makocha wao wakionyesha kombe na vyeti. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Mara ya kwanza tulianza kutoa mafunzo ya karate kwa vijana watano pekee lakini sasa tuna vijana 15 na wote ni stadi kwa mchezo huo,” alifafanua meneja huyo.

Kocha huyo alisema kuwa anaendelea kuwatayarisha vijana hao kushiriki katika mashindano ya ligi kanda ya Kati.

Alisema wazazi wote wamejitolea mhanga kuona ya kwamba wana wao wanapata vifaa vyote vinavyohitajika katika mchezo huo.

Kocha huyo ana imani ya kwamba washika dau wote wakiungana, bila shaka mchezo wa karate utaimarika eneo la Kati.

  • Tags

You can share this post!

Ripoti yapendekeza CBC ifanyiwe mageuzi makuu

Ruto ainua nyaunyo kuchapa wazembe

T L