• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 8:58 PM
Rais wa Tanzania ajitokeza kusaidia Yanga kwa hali na mali

Rais wa Tanzania ajitokeza kusaidia Yanga kwa hali na mali

JOHN ASHIHUNDU na MASHIRIKA

RAIS wa Tanzania Samia Suluhu Hassan amejitolea kwa hali na mali kuhakikisha klabu ya Young Africans (Yanga) inaweka historia kwa kuwa timu ya kwanza kutoka nchini humo kutwaa ubingwa wa Kombe la Mashirikisho barani Afrika.

“Pongezi za dhati kwa Klabu ya Yanga kwa kutinga Fainali ya Kombe la Mashirikisho. Mmeandika historia na kuiletea nchi yetu heshima kubwa sana kimataifa. Nawatakia kila la kheri katika mchezo wenu wa fainali,” rais alituma ujumbe huo kupitia kwa ukurasa wake wa mtandao wa Twitter.

Rais Suluhu Hassan ni miongoni mwa watu mashuhuri waliojitolea kusaidia klabu ya Yanga kifedha baada ya kutangaza kwamba atagharimia tiketi za mashabiki 5,000 kuingia uwanjani Jumapili kushangilia timu hiyo itakapokabiliana na USM Alger ya Algeria ugani Benjamin Mkapa kwenye mkondo wa kwanza wa mechi hiyo ya fainali.

Rais huyo aliyetimiza ahadi yake ya awali kukikabidhi timu mamilioni ya pesa kwa ushindi wao wa jumla wa 4-1 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini kwenye nusu-fainali, kadhalika ameahidi kutoa Sh1 milioni kwa kila bao watakalofungwa Jumapili na kwenye pambano la marudiano mnama Juni 3, ugenini.

Vile vile kiongozi huyo wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) ameahidi kutoa ndege maalumu ya kupeleka kikosi cha Yanga moja kwa moja nchini Algeria kwa mechi ya marudiano ya Kombe hilo kwa kimombo kama CAF Confederation Cup.

Iwapo itatwaa kombe hilo mfano wa Europa League, Yanga itakuwa klabu ya pili kutoka Afrika Mashariki kushinda taji hilo baada ya kufanya hivyo miaka 36 iliyopita.

Gor Mahia iliishinda Esperance Sportive de Tunis na kutwaa ubingwa huo mnamo 1987 wakati kombe lilijulikana kama Mandela Cup baada ya hapo awali kufahamika kama African Cup Winners Cup.

Mbele ya mashabiki wao wa nyumbani, USM Alger iliichapa ASEC Mimosas ya Ivory Coast 2-0 na kufuzu baada ya timu hizo kutoka sare 0-0 katika mkondo wa kwanza mjini Abidjan.

Yanga ambao ni mabingwa mara 29 wa Ligi Kuu ya Tanzania, wiki chache zilizopita walihifadhi ubingwa wa ligi hiyo. Aidha ndiyo klabu ya pili kutoka Tanzania kufuzu kwa nusu-fainali baada ya Simba SC kufanya hivyo mnamo 1974.

Kufikia sasa, Yanga imejikusanyia zaidi ya Sh105 kwa jumla kutoka kwa shirikisho la CAF kwa kutinga robo-fainali na nusu-fainali.

Baada ya kutoka sare 0-0 dhidi ya Rivers United ya Nigeria katika mkondo wa kwanza wa kwenye hatua ya robo-fainali, Yanga ilifuzu kwa hatua ya nusu-fainali kutokana kwa jumla ya 2-0 waliofunga katika mechi ya marudiano.

  • Tags

You can share this post!

Maina Njenga afikishwa mahakamani akidaiwa kuhusika na...

Jaji ajiondoa kuskiza kesi ya ufisadi

T L