• Nairobi
  • Last Updated March 5th, 2024 12:43 PM
Rais wa tenisi ya mezani duniani apongeza Kenya kwa kuandaa Kombe la Afrika la kufana

Rais wa tenisi ya mezani duniani apongeza Kenya kwa kuandaa Kombe la Afrika la kufana

Na GEOFFREY ANENE

RAIS wa Shirikisho la Kimataifa la Tenisi ya Mezani (ITTF) Petra Sorling amepongeza serikali ya Kenya kwa kuandaa mashindano ya kufana ya Afrika mnamo Mei 1-6.

Akizungumza katika ukumbi wa kimataifa wa michezo wa Kasarani jijini Nairobi mnamo Mei 6, raia huyo Mswidi pia amehakikishia Bara Afrika kuwa litapata usaidizi zaidi hivi karibuni.

Sorling, ambaye ni mwanamke wa kwanza kabisa kuchaguliwa rais wa ITTF, alitaja maandalizi na viwango vya mchezo vilivyooneshwa katika mashindano hayo ni vya kutia moyo sana.

“Nimefurahishwa na kile nimeona katika Kombe la Afrika la ITTF mwaka huu. Kuna hatua kubwa nzuri zimepigwa katika maandalizi na Kenya imekuwa mwenyeji mzuri. Ningependa hasa kupongeza Chama cha Tenisi ya Mezani Kenya (KTTA) chini ya uongozi wa Andrew Mudibo,” alitanguliza Sorling.

Aliongeza, “Tumeshuhudia talanta mpya kwenye mashindano haya, kutoka Uganda na Madagascar, kwa mfano. Huu ni ukuaji mzuri wa mchezo huu wetu. Tuna hamu kubwa ya kuona wachezaji zaidi wa Afrika wakifanya vyema katika kiwango cha juu kabisa. Afrika na wanachama wake 54 ni muhimu sana kwa ITTF. Afrika ina siku nzuri za usoni katika tenisi ya mezani na tutaendelea kuisaidia kupitia miradi na shughuli zetu.”

Afisa huyo mwenye umri wa miaka 52 alifurahia kuwa mashindano ya dunia yatafanyika Afrika kwa mara ya kwanza tangu 1939 hapo Mei 20-28 mjini Durban, Afrika Kusini.

Alielezea matumaini yake katika maandalizi ya mashindano ya dunia akitumai kuwa Waafrika wataongeza msisimko katika mashindano hayo.

Katika kikao hicho cha wanahabari, rais wa Shirikisho la Kimataifa la Tenisi ya Mezani barani Afrika (ITTF Africa) Khaled El-Salhy pia alisifu KTTA kwa kuandaa mashindano ya Afrika kwa mara ya pili ndani ya miaka mitano.

El-Salhy alitoa hakikisho kuwa ITTF Africa itasaidia mataifa wanachama.

Naibu rais wa ITTF, Wahid Oshodi, alisema kuwa Kombe la Afrika ni ushahidi tosha kuwa Kenya ina uwezo wa kuandaa mashindano zaidi makubwa ya kimataifa. Alisema kuwa Kenya imeonesha kujitolea kuinua mchezo huo katika kipindi cha miaka mitano sasa.

Raia huyo wa Nigeria alisema kuwa Durban kuwa mwenyeji wa mashindano ya dunia ni thibitisho kuwa pia ITTF ina imani na Afrika.

Kwa upande wake, Mudibo alishukuru ITTF kwa kusaidia Kenya katika juhudi zake za kuandaa mashindano ya kufana ya Afrika. Alisema kuwa anatumai Kenya itapata kuandaa mashindano zaidi ya kimataifa.

Mwenyekiti wa Baraza la Kitaifa la Michezo Kenya (KNSC) Nderitu Gikaria alisema kuwa mwenyeji wa mashindano ya Afrika kumepatia wachezaji wa Kenya uzoefu.

“Uzoefu ni muhimu sana kwa wachezaji wetu kuwafanya waweze kushindana kimataifa,” aliongeza Gikaria, akisema mashindano hayo kuandaliwa Kenya pia ni kitu kizuri katika kuinua utalii.

Kombe la Afrika 2023 lilivutia mataifa ya Kenya, Nigeria, Misri, Algeria, Tunisia, Cameroon, Djibouti, Uganda, Burundi na Congo Brazzaville, miongoni mwa mengine.

  • Tags

You can share this post!

Thika Queens warambwa na Vihiga Queens, Gaspo nao watandika...

MFALME CHARLES III AVIKWA TAJI: Marais waalikwa wafuatilia...

T L