NA JOHN KIMWERE
TIMU ya Re-Union FC inalenga kupambana kwa udi na uvumba kuhakikisha imenasa tiketi ya kufuzu kupandishwa ngazi kushiriki Ligi ya Taifa Daraja la Pili msimu ujao.
Kwa mara nyingine, Re-Union ambayo ni kati ya klabu kongwe nchini inashiriki Ligi ya Kanda ya Nairobi Magharibi (NWRL) baada ya kupandishwa msimu uliopita.
Kocha wake, Wilson Anjiri, anasema ndiyo amejiunga na kikosi hicho lakini baada ya kutazama wachezaji hao amegundua wanaweza kufanya vizuri ila wanahitaji kujituma na kujiaminia.
“Ni siku chache tu nimekuwa na wachezaji hawa lakini naona wanaweza pia kulingana na vile wenzangu wananieleza huenda tukiweka mpango mpya tutatimiza azma yetu,” kocha huyo alisema na kutoa wito kwa wachezaji wake kutolaza damu dimbani kwenye mechi saba zilizosalia.
Hata hivyo, katibu wake Caleb Mumbo anakiri kuwa wamepata ushindani mkali kwenye kampeni za kipute hicho muhula huu.
”Bila kujigamba tunataka kushiriki ligi ya juu msimu ujao lakini lazima tujitume kwa kuzingatia hakuna mteremko pia hakuna kizuri hupatikana rahisi,” katibu huyo amesema na kuongeza kuwa kwa asilimia kubwa ukosefu wa ufadhili umewatesa pakubwa.
Anashikilia kati ya wapinzani wao AFC Leopards Youth na Kibagare Slums ndizo zinazowanyima usingizi.
Re-Union inaorodheshwa kati ya klabu kongwe hapa nchini pia zenye historia pevu katika soka la hapa Kenya.
Klabu hii ndiyo iliyozaa Gor Mahia FC mwaka 1968 inayojivunia kushinda Ligi Kuu ya Kenya mara 19 sasa.
Naye meneja wake, Mohammed Lawi anasema kuwa viongozi Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) wanajaribu kadiri ya uwezo wao kusimamia mchezo huo.
Anawataka sana wazamie juhudi za kutafuta wadhamini kugharamia baadhi ya mahitaji ya ligi za viwango vya chini.
“Kusema kweli hata kama tungekuwa tunapata mipira kadhaa kabla ya ligi kuanza pia kulipiwa ada ya waamuzi yaani marefarii tungekuwa tunapigwa jeki pakubwa sana,” meneja huyo alisema na kuongeza kuwa pia ada ya kuleta walinda usalama uwanjani huponda klabu nyingi.
Anashikilia kuwa ni suala tete kwa kuzingatia ni sheria ya mchezo huo ambapo timu yoyote ikiwa nyumbani isipoleta maafisa wa kulinda usalama moja kwa moja hupoteza mchezo huo na kuachia alama zote tatu muhimu.
Anatoa mwito kwa wafadhili wajitokeze kuipiga jeki ili kutimiza maazimio yao ikiwamo kufuzu kushiriki ligi za hadhi ya juu nchini kama Supa Ligi ya Taifa (NSL) na Ligi Kuu ya KPL.
Re-Union FC ya sasa inajumuisha wachezaji kama: Haggai Onzere, Cordrick Otieno, Edwin ‘Campbell’ Okoth, Kevin Juma, Bramwel Were, Brian Odingo, Kephas Jairo, Edwin Naze, Titus Luyungu, Amos Nzau, Don Harrison, Calvins Ouma, Jadson Yogo na Dennis ‘Oliech’ Odhiambo. Pia wapo Caleb Maina, Martin Okeyo, Sheldon Ongenge, Joshua Omweno, Meshack Okoth, Cliff Otieno, Nimrod Harambee, Dennis Osotch, Dalton Otieno na Wycliffe ‘Lukaku’ Obel.
Klabu hii inajivunia kulea wachezaji wengi tu hapa nchini kama Jacob Kelly, Eric Masika, Ochieng Era na Joseph Shikokoti kati ya wengine.
Re-Union inajivunia kuibuka ya kwanza kubeba taji la Afrika Mashariki na Kati mara mbili mwaka 1976 na 1977.
Kadhalika iliwahi kutwaa ubingwa wa Ligi Kuu nchini mara mbili mwaka 1964 na 1975.
Mnamo 2008 na 2009 ilifanikiwa kushiriki michuano ya Ligi ya Taifa ya Daraja ya Kwanza humu nchini.