• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 12:58 PM
Robert Lewandowski mashine ya kufunga mabao

Robert Lewandowski mashine ya kufunga mabao

Na GEOFFREY ANENE>>

MSHAMBULIAJI nyota Robert Lewandowski, anayefahamika kwa wenzake kama Lewy, amekuwa mashine ya kufunga mabao kwa mwongo mzima.

Akiwa na umri wa miaka 33, nahodha huyu wa timu ya taifa ya Poland haonyeshi dalili zozote za kuanza kuwa butu.Mnamo Desemba 17, Lewandowski alifikia rekodi ya aliyekuwa mwanasoka bora duniani Cristiano Ronaldo; ya kufunga mabao mengi kutoka Januari hadi Desemba, ambayo ni 69.

Rekodi hiyo ilipatikana katika ushindi wa Bayern wa 4-0 dhidi ya Wolfsburg mnamo Desemba 17. Ronaldo alifunga 69 miaka minane iliyopita akiwa kambini Real Madrid.Lewandowski, ambaye amewania tuzo ya mwanasoka bora duniani mara nne, amepachika mabao 43 ligini 2021.

Ndiyo idadi kubwa zaidi ya mabao kuwahi kushuhudiwa kwenye Bundesliga katika kipindi cha mwaka mmoja cha kalenda ya kawaida Januari hadi Desemba. Jagina Gerd Muller ndiye alikuwa akishikilia rekodi hiyo, alipofunga mabao 42 katika mwaka mmoja mnamo 1972.

Msimu uliopita,mwanasoka huyo bora wa Poland aliibuka mfungaji bora katika msimu wa Bundesliga kwa mabao 41. Ukatili huo langoni mwa wapinzani ulimfanya kuvunja rekodi nyingine ya Muller, ya mabao 40 iliyokuwa imara kwa miaka 49.Lewy anatoka katika familia ya wanamichezo kwa hivyo talanta yake ya uchezaji ilianza kupaliliwa nyumbani.

Marehemu babake alikuwa bingwa wa judo na pia alicheza soka ligi ya daraja ya pili chini za Poland; mamake ni mchezaji mahiri wa zamani wa voliboli; dadake Milena Lewandowski-Miros pia ni mwanavoliboli shupavu na amekuwa katika timu ya taifa ya chipukizi U-21;

naye mkewe Anna Lewandowska ni mwanakarate aliyejinyakulia medali ya shaba katika mashindano ya Karate World Cup 2009. Lewandowski alianza kuhangaisha makipa mapema. Aliibuka mfungaji bora katika Ligi ya Daraja ya Pili Poland akiwa Znicz Pruszkow kwa mabao 21 katika mechi 32 msimu 2007-2008.

Aliongoza Lech Poznan kushinda Ligi Kuu (Ekstraklasa) msimu 2009-2010 alipoibuka mfungaji bora kwa mabao 18 kutokana na mechi 28.Kisha, alijiunga na Borussia Dortmund msimu 2010-2011. Tangu msimu 2011-2012, hajafunga mabao chini ya 20 ligini.

Aliibuka mfungaji bora kwa mabao 20 msimu 2013-2014 kabla ya miamba Bayern kumnyakua.Lewy anayependa sana kuendesha baiskeli na kupaisha pikipiki, alishinda tuzo ya mfungaji bora kwenye Bundesliga tena msimu 2015-2016 kwa mabao 30.

Amenyakua tuzo hiyo kwa misimu minne mfululizo sasa. Ameshinda Bundesliga mara saba akiwa Bayern na mara mbili akiwa Dortmund, na Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na Klabu Bingwa Duniani (FIFA Club World Cup) mara moja. Lewandowski amefunga mabao 19 ligini msimu huu katika mechi 17.

Pia, amefunga tisa katika michuano sita kwenye Klabu Bingwa. Ana watoto wawili wasichana – Klara Lewandowska na Laura Lewandowska.

You can share this post!

WANDERI KAMAU: Ni ukiukaji mkubwa wa katiba kudhalilisha...

Ushindani mkali Team Kenya nusra umfanye awakimbilie Bahrain

T L