• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Rotich adhihirishia Kinyamal nani mfalme wa mbio za mita 800

Rotich adhihirishia Kinyamal nani mfalme wa mbio za mita 800

Na AYUMBA AYODI

Mshindi wa medali ya shaba ya Riadha za Dunia ya mbio za mita 800 Ferguson Rotich alibwaga bingwa wa Jumuiya ya Madola Wycliffe Kinyamal akishinda mbio hizo za mizunguko miwili kwenye duru ya tatu na mwisho ya kupokezana vijiti uwanjani Nyayo, Jumamosi.

Rotich kutoka timu ya Golazo alidhihirisha nani mfalme katika umbali huo kwa kuukamilisha kwa dakika 1:45.64 na kupungia mashabiki mkono kusherehekea ushindi wake dhidi ya Kinyamal (Kaptagat) aliyemaliza kwa dakika 1:46.09.

Abel Kipsang kutoka Ngong aliridhika katika nafasi ya tatu (1:46.36), huku mshindi wa nishani ya shaba ya mashindano ya Bara Afrika ya chipukizi mwaka 2011 Jeremiah Mutai akakamilisha katika nafasi ya nne (1:47.27) katika kundi la tatu.

“Nilihisi vizuri kushinda kundi langu kwa muda huo mzuri na sikuwa na budi kushukuru mashabiki wangu baada ya kuwasikia wakinichochea,” alisema Rotich, ambaye ametangaza vita dhidi ya bingwa wa sasa wa mbio za mita 800 Donavan Brazier kutoka Amerika kabla ya michezo ya Olimpiki mjini Tokyo, Japan baadaye mwaka 2021.

Rotich alifichua kuwa mazoezi yake yameimarika baada ya kuamua kuyaanza mapema kuliko misimu iliyopita.

“Nilianza maandlizi yangu Desemba tofauti na hapo awali nilipoyaanza Januari kwa sababu mimi sishiriki mashindano ya ukumbini,” alisema Rotich, ambaye mbali na kulenga ufanisi Olimpiki baada ya kukamata nafasi ya nne mjini Rio de Janeiro mwaka 2016, anataka kupunguza muda wake bora hadi chini ya dakika 1:42.

Mtimkaji huyo anajivunia kasi yake nzuri kwenye mbio za mita 800 ya dakika 1:42.54 aliyopata mjini Monaco katika Riadha za Diamond League mwaka 2019.

“Nahisi niko katika hali nzuri kuliko miaka iliyopita na nataka kuona jinsi msimu utakavyoniendea. Nataka kukamilisha umbali huo kwa dakika 1:41 pengine mjini Monaco mwaka huu,” alisema Rotich, 31, ambaye pia anamezea mate kupeperusha bendera ya Kenya kwenye Riadha za Dunia za kupokezana vijiti nchini Poland.

Baada ya duru hiyo ya tatu, wakimbiaji sasa wanaelekeza nguvu zao kwa mashindano ya kitaifa ya kuchagua timu ya Kenya itakayoelekea Poland ambayo yatafanyika Machi 26-27 uwanjani Nyayo. Riadha za dunia zitakuwa Mei 1-2 mjini Silesia, Poland.

“Mimi ni kama mvinyo unaokuwa mzuri unapoendelea kukaa. Siwezi kukuambia nitastaafu hivi karibuni kwa sababu nalenga kushiriki Olimpiki za Tokyo mwaka huu pamoja na zile za Paris mwaka 2024,” alisema. “Siri ni kukula vizuri na kufanya mazoezi mazuri.”

Jonathan Kitilit kutoka Idara ya Majeshi (KDF) alishinda kundi la kwanza kwa dakika 1:48.902 akilemea Leny Lokitash (Ngong’) 1:49.69 naye Kipng’etich Ng’eno alitawala kundi la tatu (1:47.54).

Mshindi wa taji la kinadada la Continental Cup mbio za mita 1,500 Winny Chebet (KDF) alibwaga bingwa wa kitaifa wa mbio za mita 400 Mary Moraa akishinda mbio za mita 800 kwa dakika 2:03.72. Moraa, ambaye hana timu, alimaliza katika nafasi ya pili (2:04.32) naye Mueni Karimi kutoka Ngong akafunga mduara wa tatu-bora (2:08.16).

Hata hivyo, Moraa aling’ara katika mbio za mita 400 akiandikisha muda bora kwenye mashindano hayo ya Shirikisho la Riadha Kenya (AK) msimu huu kwa sekunde 52.63. Gladys Musyoki (Police) alitimka 54.65 akifuatiwa na Anne Mbatha (Ndura) 55.52 na Sylvia Chesebe (Prisons) 55.60.

Zablon Ekwam (Ndura) alitawala mbio za mita 400 kwa upande wa wanaume kwa sekunde 45.97 akifuatwa kwa karibu na Emmanuel Mutua (Southern) na William Ryan (Police) kwa sekunde 46.35 na 46.63, mtawalia.

Maximilla Imali (Police) alionyesha wapinzani wake wa mbio za mita 200 kivumbi akitwaa ushindi kwa sekunde 24.54. Tazan Kamanga (TKD) alitimka kasi ya juu katika kitengo cha wanaume alichokamilisha kwa sekunde 20.71 mbele ya Mark Otieno (20.86). – TAFSIRI ya GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Wanaraga wa Machine wazidia nguvu Egerton Wasps

Kenya waingia Kombe la Afrika la hoki bila jasho baada ya...