• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
Rovanpera, Ogier waingia Safari Rally

Rovanpera, Ogier waingia Safari Rally

Na GEOFFREY ANENE

BINGWA wa dunia Kalle Rovanpera ni miongoni mwa madereva wanane kutoka timu ya Toyota Gazoo waliothibitisha kushiriki raundi ya saba ya Mbio za Magari Duniani (WRC) Safari Rally nchini Kenya mnamo Juni 22-25.

Zoezi la kutoa ithibati ya kushiriki ilifunguliwa Mei 1.

Rovanpera, ambaye pia ni bingwa mtetezi wa Safari Rally, atashirikiana na mwelekezi wake wa kawaida Jonne Halttunen pia kutoka Finland katika gari la Toyota Yaris GR R1 Hybrid.

Gari hilo limetawala raundi tatu kati ya nne ambazo zimeshafanywa.

Mfaransa Sebastien Ogier aliyeshinda Safari Rally 2021, alipatia Toyota ushindi wa kwanza katika raundi ya kwanza mjini Monte Carlo, Monaco na pia akatawala raundi ya tatu nchini Mexico akishirikiana na Vincent Landais, ni dereva mwingine aliyejiandikisha.

Madereva wengine watakaopaisha magari ya Toyota Yaris katika Safari Rally 2023 ni Muingereza Elfyn Evans aliyebeba taji la Croatia Rally mwezi Aprili, na Mjapani Katsuta Takamoto aliyekamata nafasi ya pili katika Safari Rally 2021.

Safari Rally itaanzia katika bustani ya Uhuru Park na kuwa na mkondo mmoja katika mashamba ya kituo cha kimataifa cha Kasarani. Itaelekea kaunti ya Nakuru ambapo sehemu kubwa ya mashindano hayo itaandaliwa katika eneobunge la Naivasha.

Madereva wengine waliothibitisha kushiriki ni Jason Bailey na James Willets kutoka Canada watakaopeleka magari ya Ford Fiesta R3 yanayotumiwa pia na chipukizi wa Kenya, wakiwemo Hamza Anwar na Jeremiah Wahome.

Martin Prokop akielekezwa na raia mwenzake kutoka Czech, Zdenek Jurka, wataendesha Ford Fiesta MK1 R2.

Mkenya Minesh Rathod na mwelekezi wake Jamie McTavish kutoka Uingereza watashirikiana katika gari la Mitsubishi Lancer EVO10.

Yeye ndiye dereva wa kwanza kujiandikisha kushiriki kitengo cha Mbio za Magari za Kitaifa Kenya (KNRC) kitakachokuwa sehemu ya WRC Safari Rally.

Orodha hiyo ya kwanza ya madereva imethibitishwa na msimamizi wa Safari Rally, Gurvi Bhabra.

Ogier anaongoza WRC 2023 sako kwa bako na Evans (pointi 69) wakifuatiwa na Rovanpera (68) na Ott Tanak kutoka timu ya Ford (65).

Madereva waliothibisha kufikia Mei 5 ni:

Kalle Rovanpera/Jonne Halitunen (Toyota Yaris Hybrid R1)

Elfyn Evans/Scott Martin (Toyota Yaris Hybrid R1)

Sebastien Ogier/Vincent Landais (Toyota Yaris Hybrid R1)

Takamoto Katsuta/Aaron Johnston (Toyota Yaris Hybrid R1)

Minesh Rethod/Jamie McTavish (Mitsubishi EVO10)

Karan Patel/Tausef Khan (Ford Fiesta R2)

Martin Prokop/ Zdenek Jurka (Ford Fiesta MK1 R2)

Jasen Bailey/James Willets (Ford Fiesta RC3)

  • Tags

You can share this post!

Shakahola: Ufukuaji miili kurejelewa baada ya kukamilika...

Mhubiri mwingine Kilifi naye atiwa mbaroni sababu msichana...

T L