• Nairobi
  • Last Updated October 1st, 2023 9:40 PM
Ruto, Raila wapongeza Faith Kipyegon kwa kuweka rekodi mpya ya dunia

Ruto, Raila wapongeza Faith Kipyegon kwa kuweka rekodi mpya ya dunia

Na GEOFFREY ANENE

NYOTA wa mbio za mita 1,500 Faith Chepng’etich Kipyegon amemininiwa sifa tele baada ya kufuta rekodi ya dunia ya 5000m kwenye riadha za Diamond League jijini Paris, Ufaransa, Ijumaa usiku.

Chepng’etich aliweka rekodi ya dunia ya 1,500m ya dakika 3:49.11 kwenye Florence/Roma Diamond League mnamo Juni 2 baada ya kufuta ya Muethiopia Genzebe Dibaba ya 3:50.07 iliyokuwa imara tangu 2015.

Hapo Ijumaa, Chepng’etich, ambaye mara ya mwisho alikuwa ameshiriki 5,000m ni mwaka 2015, alinyakua taji la Paris Diamond League la umbali huo kwa dakika 14:05.20 akivunja rekodi ya Letesenbet Gidey ya 14:06.62. Muethiopia Gidey aliweka rekodi mjini Valencia, Uhispania mwaka 2020.

Katika mitandao ya kijamii, Rais William Ruto aliandika kuwa msukumo, umakinifu, kiu ya kutafuta mafanikio na mtazamo wa ushindi ni fomula ya ukuu.

“Faith Kipyegon amefanya mambo tena. Rekodi nyingine ya dunia, mara hii katika 5,000m. Hakika ni mwanariadha mzuri! Motisha isiyo na kifani! Hongera! Kenya inajivunia kazi yako!” alisema Rais Ruto.

Mwanasiasa mkongwe Raila Odinga alifurahishwa na rekodi mpya ya Chepng’etich iliyopatikana wiki moja baada ya ile ya 1500m.

“Faith Kipyegon amevunja rekodi ya dunia ya 5000m katika muda wa kustaajabisha wa 14:05.20 na kuandikisha historia tena! Hongera!” alisema.

Mama wa Taifa Rachel Ruto aliwapongeza Faith Kipyegon na mshindi wa mbio za mita 800 Emmanuel Wanyonyi kwa kazi yao safi jijini Paris.

“Wanyonyi alishinda 800m kwa muda bora mwaka huu duniani naye Kipyegon akavunja rekodi ya dunia ya 5000m. Ushindi wao unafurahiwa kote nchini. Kenya inajivunia mafanikio yao. Wao sio tu wanariadha wa kipekee, bali pia ni motisha kwa wale walio na ndoto kubwa,” alisema.

Mawaziri Ababu Namwamba (Vijana, Michezo na Sanaa) na Kipchumba Murkomen (Uchukuzi) pia walipongeza na kumsherehekea wanariadha hao pamoja na bingwa wa Afrika na Jumuiya ya Madola mbio za 100m Ferdinand Omanyala aliyekamata nafasi ya pili kwa sekunde 9.98, nyuma ya Mwamerika Noah Lyles (9.97).

  • Tags

You can share this post!

Fainali ya Klabu Bingwa Ulaya: Guardiola asipobeba taji...

Uingereza kuwakilishwa na vikosi vinane kwenye soka ya bara...

T L