• Nairobi
  • Last Updated May 24th, 2024 12:59 PM
Safari ya Arsenal kwenye UEFA msimu huu yakatizwa na vipusa wa Wolfsburg kwenye robo-fainali

Safari ya Arsenal kwenye UEFA msimu huu yakatizwa na vipusa wa Wolfsburg kwenye robo-fainali

Na MASHIRIKA

ARSENAL walidenguliwa kwenye robo-fainali za Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu baada ya Wolfsburg ya Ujerumani kuwapokeza kichapo cha jumla ya mabao 3-1.

Vipusa wa Arsenal walishuka dimbani kwa mechi ya marudiano nchini Ujerumani mnamo Machi 31, 2022 baada ya kuambulia sare ya 1-1 katika mkondo wa kwanza ugani Emirates, Uingereza.

Jill Roord ambaye ni mwanasoka wa zamani wa Arsenal aliwaweka Wolfsburg kifua mbele kabla ya beki Leah Williamson kujifunga alipobabatizwa na mpira kutoka kwa Sveindis Jane Jonsdottir katika dakika ya 72. Wolfsburg waliokuwa wakichezea katika uwanja wao wa nyumbani wa Volkswagen Arena wangalifunga mabao zaidi katika kipindi cha pili.

Goli Tabea Wassmuth kwa upande wa Wolfsburg halikuhesabiwa baada ya teknolojia ya VAR kubainisha kwamba alicheka na nyavu za Arsenal akiwa ameotea. Juhudi za Arsenal kurejea mchezoni ziligonga mwamba huku kombora la Vivianne Miedema likigonga mhimili wa goli naye Williamson akazidiwa ujanja na kipa wa Wolfsburg, Almuth Schult.

Wolfsburg sasa watakutana na Barcelona waliofuzu kwa nusu-fainali mnamo Machi 30, 2022 kwa kukomoa watani wao wa tangu jadi Real Madrid kwa jumla ya mabao 8-3. Mechi ya mkondo wa pili kati ya Barcelona na Real ulihudhuriwa na mashabiki 91,533 na idadi hiyo ikaweka historia ya mahudhurio ya mechi katika historia ya klabu hizo.

Uingereza sasa haina mwakilishi yeyote kwenye UEFA msimu huu baada ya Wolfsburg waliotawazwa mabingwa wa kipute hicho mnamo 2011-12 na 2013-14 mfululizo kudengua Arsenal.

Huku Arsenal wakipigania taji la Ligi Kuu ya Uingereza (WSL), Wolfsburg pia wanafukuzia ubingwa wa Ligi Kuu ya Ujerumani na kwa sasa wanashindia Bayern Munich kwa pointi moja pekee kileleni mwa jedwali. Ni pengo la alama moja pekee pia ambalo linawatenganisha Chelsea na Arsenal wanaoselelea kileleni mwa jedwali la WSL.

Arsenal walionyanyua ubingwa wa UEFA mnamo 2007, walitinga nusu-fainali za kipute hicho mara ya mwisho miaka tisa iliyopita. Kikosi hicho kinawania pia taji la Kombe la FA msimu huu na watakutana na Chelsea kwenye nusu-fainali mnamo Aprili 2022.

You can share this post!

Wapigakura wafu 250,000 kutupwa

Kalonzo apanga UhuRaila

T L