• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 6:27 PM
Sergio Busquets kuagana na Barcelona baada ya miaka 18 ugani Camp Nou

Sergio Busquets kuagana na Barcelona baada ya miaka 18 ugani Camp Nou

Na MASHIRIKA

NAHODHA Sergio Busquets amethibitisha kwamba ataagana rasmi na Barcelona mwishoni mwa msimu huu wa 2022-23 baada ya kuhudumu kambini mwa miamba hao wa Uhispania kwa kipindi cha miaka 18.

Kiungo huyo wa zamani wa Uhispania mwenye umri wa miaka 34 amewajibikia Barcelona mara 718, idadi hiyo ya mechi ikimweka katika nafasi ya tatu kwenye orodha ya wanasoka ambao wamechezea kikosi hicho mara nyingi zaidi katika historia.

Miongoni mwa mataji ambayo Busquets ameshindia Barcelona katika kipindi hicho ni manane ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga), saba ya Copa del Rey, saba ya Spanish Super Cup na matatu ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA).

“Ingawa hayajakuwa maamuzi mepesi, nadhani muda wa kuondoka umefika. Imekuwa safari ndefu ambayo siwezi kabisa kuisahau. Ilikuwa ndoto yangu ya tangu utotoni kuvalia jezi za Barcelona nikichezea ugani Camp Nou,” akasema Busquets.

Busquets aliingia katika sajili rasmi ya Barcelona mnamo 2005 akiwa tineja. Alijikuza katika akademia ya miamba hao na akafaulu kuunga kikosi cha pili na kuwajibikia Barcelona B kwa mara ya kwanza chini ya kocha Pep Guardiola dhidi ya Racing Santander mnamo 2008.

Busquets, ambaye ni kiungo mkabaji, atatamatisha taaluma yake kambini mwa Barcelona akijivunia kunyanyua taji la tisa la La Liga mwishoni mwa msimu huu.

Kufikia sasa, masogora hao wa kocha  Xavi Hernandez wanaselelea kileleni mwa jedwali la La Liga kwa alama 13 zaidi kuliko nambari mbili Atletico Madrid huku zikisalia mechi tano pekee kabla ya msimu huu kukatika rasmi.

Katika kipindi cha zaidi ya miaka 15 akivalia jezi za Barcelona, Busquets amefunga mabao 18 na kuchangia 40 mengine.

Nahodha huyo wa zamani wa Uhispania alistaafu soka ya kimataifa mnamo Disemba akijivunia kushindia kikosi hicho Kombe la Dunia la 2010 na ubingwa wa Euro 2012.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Mkuu Kemsa aweka wazi asilimia ya wafanyakazi kwa kuangalia...

Maajabu mashemeji wakicharaza baba ya mume

T L