• Nairobi
  • Last Updated April 25th, 2024 1:47 PM
Shujaa kuanza vita vya kuponea shoka dhidi ya Canada Raga za Dunia jijini London

Shujaa kuanza vita vya kuponea shoka dhidi ya Canada Raga za Dunia jijini London

Na GEOFFREY ANENE

DROO ya duru ya mwisho ya Raga za Dunia 2022-2023 imetangazwa ambapo Kenya Shujaa itaanza kampeni ya kukwepa kutemwa dhidi ya Canada mjini London, Uingereza.

Vijana wa kocha Damian McGrath watakabana koo na Canada mnamo Mei 20 saa nane kasoro dakika tisa mchana ugani Twickenham.

Wakenya, ambao wameshiriki duru zote za Raga za Dunia tangu msimu 2002-2003, watalimana na washindi wa Challenger Series Tonga (4.59pm) siku hiyo kabla ya kumaliza mchujo huo wa mataifa manne dhidi ya Uruguay mnamo Mei 21 (2.19pm).

Mshindi kutoka orodha ya Kenya, Canada, Uruguay na Tonga atashiriki duru zote kwenye ligi hiyo ambayo timu zitapunguzwa kutoka 15 hadi 12 msimu ujao.

Shujaa ilijipata katika vita hivyo baada ya kumaliza duru 10 za msimu 2022-2023 katika nafasi ya 13 kwa alama 40. Uruguay walikamata nafasi ya 12 kwa alama 54 nao Canada wakawa nambari 14 kwa alama 39.

Japan waliovuta mkia walitemwa moja kwa moja, huku Tonga ikipata tiketi ya mashindano hayo ya mataifa manne kwa kushinda Challenger Series.

New Zealand (pointi 186), Argentina (159), Ufaransa (139), Fiji (138), Australia (125), Samoa (116), Afrika Kusini (116), Ireland (104), Amerika (95), Great Britain (94) na Uhispania (55) watashiriki duru zote msimu ujao kwa sababu walimaliza duru 10 za kwanza za msimu 2022-2023 katika nafasi 11 za kwanza.

  • Tags

You can share this post!

Wakili aomba ICC ichunguze mauaji ya Shakahola

Umuhimu na faida ya magnesiamu mwilini

T L