• Nairobi
  • Last Updated February 26th, 2024 10:50 AM
Simiu apasha misuli moto akimezea mate mamilioni ya Delhi Half Marathon

Simiu apasha misuli moto akimezea mate mamilioni ya Delhi Half Marathon

Na GEOFFREY ANENE

MKENYA Daniel Simiu ameingia katika kinyang’anyiro cha Vedanta Delhi Half Marathon nchini India ambapo kuna tuzo ya Sh5,715,450 kwa mshindi atakayeweka rekodi mpya hapo Oktoba 15.

Tuzo ya kumaliza mbio hizo za kilomita 21 ni Sh3,956,850. Mshindi akipata taji kwa kufuta rekodi za Delhi Half Marathon za Waethiopia Amedework Walelegn (dakika 58:53) na Yalemzerf Yehualaw (saa 1:04:46), ataongezwa Sh1,758,600.

Simiu alinyakua medali ya fedha katika mbio za mita 10,000 kwenye Riadha za Dunia nchini Hungary mnamo Agosti 20.

Amejumishwa katika timu ya Kenya ya Riadha za Dunia za Barabarani zitakazofanyika Septemba 30 hadi Oktoba 1 nchini Latvia.

Simiu anajivunia muda bora wa dakika 59 na sekunde nne katika nusu-marathon kutoka nambari mbili alipata katika Bahrain Royal Night Half Marathon jijini Manama.

Jijini Delhi, Simiu anatarajiwa kupata ushindani mkali kutoka kwa Wakenya Leonard Barsoton (59:09), Isaac Kipkemboi (59:17), Isaia Lasoi (59:27) na Roncer Konga (59:38), Waethiopia Tesfahun Akalnew (59:22), Gemechu Dida (59:53), Boki Diriba (60:34), Demeke Tesfaye (61:37) na Kuma Dejene (64:38) na Samsom Amare kutoka Eritrea (60:08).

Kitengo cha wanawake kimevutia Mkenya Viola Chepngeno (66:48) na Waethiopia Almaz Ayana (65:30), Betelihem Afenigus (66:46), Bertukan Welde (67:44), Alem Nigussie (67:50), Dawit Seyaum (67:52) na Mganda Stella Chesang (68:11).

Almaz aliibuka mshindi mwaka 2017 kwa hivyo atakuwa akivizia taji lake la pili.

  • Tags

You can share this post!

Mahakama yadumisha uamuzi wa kutimuliwa kwa jaji mwenye...

Aibu Kenya ikilimwa na Sudan Kusini nyumbani Kasarani

T L