• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
Simiu ni mfalme mpya wa Kip Keino Classic mita 10000

Simiu ni mfalme mpya wa Kip Keino Classic mita 10000

Na GEOFFREY ANENE 

MSHINDI wa medali ya fedha ya Jumuiya ya Madola Daniel Simiu alisisimua mashabiki kwenye Riadha za Kip Keino Classic Continental Tour ugani Kasarani, Jumamosi.

Simiu alitawala mbio za mita 10,000 kwa dakika 28:09.93. Alifyatuka ikisalia mizunguko miwili na kufungua mwanya wa 500m.

“Ushindi leo ni ishara ya msimu mzuri na ninafurahia kuanza vyema. Mpango wangu mkubwa ni kufuzu kushiriki Riadha za Dunia mjini Budapest, Hungary kwa sababu hicho ni kilele cha mashindano ya mbio. Nahisi raha kushinda hapa mbele ya mashabiki wa hapa nyumbani,” alisema Simiu aliyefuatwa kwa karibu na Edwin Kipkemoi (28:30.05) na Stanley Njihia (28:30.61).

Bingwa wa Jumuiya ya Madola mbio za 5000m, Beatrice Chebet aling’ara katika kitengo hicho kwa dakika 15:15.82.

Afisa huyo wa polisi aliwaonesha kivumbi Margaret Kipkemboi (15:16.28) na Judith Kiyeng (16:16.66).

Mbelgiji Timothy Herman aliyekuwa nambari mbili mwaka 2021, aliweka rekodi mpya ya kurusha mkuki ya Kip Keino Classic baada ya kushinda taji kwa mita 87.35.

Bingwa mara mbili wa dunia Anderson Peters (Grenada) aliridhika na medali ya fedha (85.72m) na mshindi wa mwaka 2022 Mmisri Ihab Abdelramah (81.04m). Mkenya Julius Yego alikamata nafasi ya tano (77.24m).

Isaac Kirwa na Peter Kamau walivuna mataji ya kuruka umbali na kutupa tufe baada ya kuandikisha 7.34m na 16.25m, mtawalia.

Wiseman Were aliweka rekodi mpya ya Kip Keino Classic katika mbio za 400 kuruka viunzi ya sekunde 49.59 na kufuzu kushiriki Riadha za Dunia mjini Budapest, Hungary mwezi Agosti.

Taji la 400m kuruka viunzi la wanawake liliendea Hannah Mwangi (sekunde 57.44) akifuatiwa na Diana Chebet (59.40) na  Jane Chege (59.97).

Aaron Brown kutoka Canada na mwanadada Sha’Carri Richardson kutoka Amerika walishinda mbio za mita 200 naye Mwamerika Twanisha Terry akatawala 100m kwenye mashindano hayo yaliyovutia mashabiki kiasi cha haja.

  • Tags

You can share this post!

Absa Kip Keino Classic: Ferdinand Omanyala ahifadhi taji...

Nassir apinga kulipa deni la maziwa shuleni

T L