• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 10:55 AM
SJAK na LG wasaini kandarasi ya Sh3.5m kutuza wanamichezo bora Kenya

SJAK na LG wasaini kandarasi ya Sh3.5m kutuza wanamichezo bora Kenya

Na GEOFFREY ANENE

CHAMA cha Waandishi wa habari za michezo nchini Kenya (SJAK) kimesaini kandarasi mpya na kampuni ya vifaa vya kielektroniki ya LG East Africa mnamo Jumatatu kuendelea kudhamini tuzo ya mwanamichezo bora wa mwezi.

Kandarasi hiyo inayoweza kuongezwa baada ya mwaka ni ya Sh3.5 milioni. Ilianza Januari 2023 hadi Desemba 2023.

Tuzo ya LG/SJAK inalenga kuzawadia wanamichezo wa Kenya kutoka fani mbalimbali waliong’ara kila mwezi.

Akizungumza katika hafla ya kusaini kandarasi mjini Nairobi, Mkurugenzi Mkuu wa LG, Dong Won Lee amesifu ushirikiano wa muda mrefu kati ya pande hizo akisema kuwa utachangia pakubwa katika kukuza michezo nchini Kenya kwa kutuza talanta.

“Kwa muda mrefu, wanariadha wa Kenya wamefanya vyema hapa Afrika na duniani. Kutambulika kwa kazi yao ni hatua muhimu katika kutambua na kukuza talanta hapa nchini. Ni muhimu kutuza wanariadha wetu wa mbio fupi na masafa ya kadri pamoja na wanamichezo kutoka fani nyingine waliofanya vyema,” amesema Lee.

Washindi wa tuzo hiyo wataamuliwa na jopo la majaji saba walioteuliwa na SJAK na watapata bidhaa tofauti kutoka kwa LG.

Baadhi ya tuzo wanamichezo bora watapata kila mwezi mwaka 2023 ni runinga ya LG NanoCell inayotoa picha safi na sauti pamoja na mashine ya kisasa ya kufua nguo ya LG AI DD.

Wanamichezo bora wa Januari, Februari, Machi na Aprili watatuzwa kabla ya mwezi huu wa Mei kukamilika.

Kwa upande wake, rais wa SJAK, James Waindi, amesema kuwa tuzo hiyo itaendelea kuwapa motisha wanamichezo wa Kenya ambao wamepitia changamoto nyingi tangu janga la Covid-19 lianze mwaka 2020.

“Ushirikiano huu na LG ambao umekuwa kwa zaidi ya miaka minane, utaendelea kutupatia mazingira mazuri kwa wanamichezo kutoka mashinani kung’ara kimataifa. Tunapanua tuzo hii ili tuwe na fani nyingi ili talanta tofauti zipate kuonekana,” amesema Waindi.

Isitoshe, Waindi amesisitiza umuhimu wa michezo katika maendeleo ya kijamii, kiuchumi na kitamaduni.

“Kuwekeza katika michezo pia kuna manufaa mengi kwa vijana kwa sababu ni njia pia ya kupata mapato na fursa ya kibiashara,” akasema Waindi.

  • Tags

You can share this post!

TSC: Walimu walioajiriwa kwa kandarasi wasubiri kazi ya...

MAPISHI KIKWETU: Kuku choma, paprika, mdalasini na dengu

T L