• Nairobi
  • Last Updated June 2nd, 2023 9:28 PM
Soka: Fahamu jinsi Kinale Girls inavyojiandaa kwa ajili ya mashindano ya mwaka 2023

Soka: Fahamu jinsi Kinale Girls inavyojiandaa kwa ajili ya mashindano ya mwaka 2023

NA LAWRENCE ONGARO

SHULE ya upili ya wasichana ya Kinale Girls, kaunti ya Kiambu, inajipanga kivingine ili kurejea na mbinu geni katika soka mwaka 2023.

Kocha wa shule hiyo Ben Nyongesa, amewasajili vipusa wanane wapya watakaoleta uhai kikosini.

“Huku wanafunzi wachache wa Kidato cha Nne wakikamilisha muhula wao wa masomo, ni vyema kujipanga mapema,” alisema kocha huyo.

Baadhi ya nyota hao wanane wanaojiseti kujiunga na akina dada wengine wa Kinale Girls ni Stecy Aoko, Agnes Kusaka, Mildred Moraa, Ruth Chepketer, Mercy Chemeli, Sheril Atieno, Cynthia Akinyi na Gladys Mbula.

Akizungumza kwa kirefu na Taifa Spoti katika uga wao wa shule, kocha huyo alisema msimu ujao wa 2023, utakuwa tofauti kabisa.

Alisema msimu uliopita walishiriki katika michezo ya kitaifa ya shule za upili iliyofanyika jijini Nakuru mwezi Septemba 2022.

Alisema walibanduliwa katika robo fainali na shule ya upili ya Itigo Girls kwa kupigwa magoli 3-0.

Hata hivyo anasema alipata majeruhi kadha katika hatua ya mwisho jambo lililoponza juhudi zao za kutaka kusonga mbele.

Shule ya upili ya wasichana ya Kinale Girls, kaunti ya Kiambu, inajipanga kivingine ili kurejea na mbinu geni katika soka mwaka 2023. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Kocha huyo anapongeza mwalimu mkuu wa shule hiyo Bulfrida Simiyu kwa kuwapa sapoti yote wanayohitaji.

“Akina dada hawa wamenunuliwa vifaa vyote vya michezo na kwa hivyo wanastahili kuvuta kutia bidii,” alieleza Nyongesa.

Naye Mwalimu Simiyu alisema wanatoa wito kwa wahisani wafanye hima ya kuwanunulia basi la shule ili wasichana hao wapate njia rahisi ya usafiri.

“Ningetamani wasichana wangu watambe kwa masomo na michezo sambamba ili shule yangu iweze kutambulika kwenye ramani ya Kenya na kwingineko,” alieleza Mwalimu mkuu Simiyu.

Simiyu alisema akina dada hao pia wanaandikisha matokeo mazuri katika mitihani yao.

  • Tags

You can share this post!

Matibabu: Minet yaagizwa isuluhishe mzozo wake na walimu

Ruto ajipatia njia kukwepa kosa la Uhuru

T L