• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 1:29 PM
Soka yahamia Uarabuni CR7, Benzema wakiendea mihela

Soka yahamia Uarabuni CR7, Benzema wakiendea mihela

Na CHRIS ADUNGO

MASHABIKI wa soka wameanza kuhisi kwamba upo wakati ambapo Ligi Kuu ya Saudi Arabia itaanza kuwa kivutio kikubwa kama ilivyo Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) kwa sasa.

Mtazamo wao huo unachochewa na tukio la kuongezeka kwa idadi ya wanasoka wa haiba kubwa wanaojiunga na vikosi mbalimbali vya Ligi Kuu ya Saudia.

“Wacha wanasoka waende huko kutengeneza hela. Wakati utafika ambapo soka ya Saudia itavutia zaidi kuliko hata ya Uingereza. Uarabuni sasa ndiko kwenye dili,” akasema Makambo Bingwa ambaye ni miongoni mwa marafiki zangu Facebook.

“Lakini je, unashabikia timu gani huko Uarabuni?” akadakia rafiki yangu mwingine kwenye mtandao huo, Stephen Ogeng’o Bwire.

Ingawa marafiki zangu hawa waliahidi kuendeleza mjadala huo kwenye jukwaa jingine tofauti, naungama kuwa kuna ongezeko la idadi ya masogora wa haiba kubwa wanaozidi kutua Saudi Arabia ambao wanapigiwa upatu wa kuwa wenyeji wa fainali za Kombe la Dunia 2030.

Hata hivyo, maoni ya Bw Makambo kuwa wachezaji hawa wanajiunga na klabu za Uarabuni ili ‘kutengeneza’ pesa yanazua mjadala mwingine wa iwapo hakuna pesa huko walikotokea na wanakozidi kutokea wanasoka hao. Sehemu ya mjadala huo itajibiwa katika makala haya:

KARIM BENZEMA

Mshindi huyo wa Ballon d’Or amekubali kujiunga na Al-Ittihad ambao ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Saudi Arabia kwa mkataba wa miaka mitatu baada ya kuagana rasmi na Real Madrid ya Uhispania.

Hadi alipobanduka ugani Bernabeu, Benzema, 35, alikuwa ameshindia Real jumla ya mataji 25 katika kipindi cha miaka 14. Kati ya makombe hayo ni matano ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) na manne ya Ligi Kuu ya Uhispania (La Liga).

Kwa mujibu wa kocha Carlo Ancelotti, ofa ya mshahara mnono ambao Benzema aliahidiwa na Al-Ittihad ilikuwa kiini cha Real kumwachilia licha ya kusalia na mwaka mmoja zaidi kwenye mkataba wao naye.

“Mbali na Benzema, Real wamekatiza pia uhusiano na Eden Hazard, Marco Asensio na Mariano Diaz. Kubanduka kwa wanne hao kunapunguzia kikosi gharama ya matumizi kwa hadi Sh11.4 bilioni,” akatanguliza Ancelotti.

“Sasa wanahemea huduma za Harry Kane ambaye Tottenham Hotspur wamedokeza kuwa hauzwi chini ya Sh17 bilioni. Huenda Real wakafikiria kununua mwanasoka mwingine kwa bei ndogo iwapo Spurs watakaa kushuka,” akaelezea gazeti la Marca.

Iwapo wataambulia pakavu katika juhudi zao za kumsajili Kane, Real watawania maarifa ya Victor Osimhen (Napoli), Lautaro Martinez (Inter Milan), Kai Havertz (Chelsea) Dusan Vlahovic wa Juventus.

Benzema, 35, aliondoka Real baada ya kuwafungia mabao 354 yanayomweka nyuma ya Cristiano Ronaldo kwenye orodha ya wafungaji bora wa muda wote katika kikosi hicho.

Ronaldo, aliyepachika wavuni magoli 450, sasa anasakatia kikosi cha Al-Nassr katika Ligi Kuu ya Saudi Arabia.

“Ni ligi nzuri ambayo tayari inajivunia wachezaji wazuri. Ronaldo yuko kule tayari. Yeye ni rafiki yangu na ni sogora mkubwa duniani. Hiyo ni ithibati tosha kwamba Saudi Arabia wamejitolea kufikisha soka katika kiwango tofauti cha ushindani. Niko hapa kuendeleza taaluma yangu na kushinda mataji sawa na nilivyozoea kufanya bara Ulaya,” akasema Benzema.

Kikosi cha Al-Ittihad kwa sasa kinanolewa na kocha wa zamani wa Wolverhampton Wanderers na Spurs, Nuno Espirito Santo.

Benzema aliwajibishwa na Real katika mechi 648 tangu mwaka wa 2009 alipobanduka kambini mwa Olympique Lyon ya Ufaransa. Tofauti na Sh6.6 bilioni alizokuwa akila kwa mwaka ugani Bernabeu, Benzema sasa atakuwa akidumishwa kwa mshahara wa Sh17.8 bilioni kwa mwaka kambini mwa Al-Ittihad.

Mnamo Juni 5, ilitangazwa kwamba Al-Ittihad ni miongoni mwa vikosi vinne vikuu vya Saudi Arabia ambavyo umiliki wao umetwaliwa na Hazina ya Uwezekaji wa Umma (PIF) ambayo pia inamiliki kikosi cha Newcastle United nchini Uingereza.

Kikosi kingine ni Al-Nassr inayomhifadhi Ronaldo na Al-Hilal wanaohusishwa na uwezekano mkubwa wa kumsajili Lionel Messi wa Paris Saint-Germain (PSG) muhula huu.

CRISTIANO RONALDO

Supastaa huyo raia wa Ureno ndiye mwanasoka anayedumishwa kwa mshahara mnono zaidi duniani baada ya kuagana na Manchester United mnamo 2022 na kutia saini mkataba wa kuchezea Al Nassr ya Saudi Arabia hadi 2025.

Kwa sasa analipwa Sh26.4 bilioni kwa mwaka, ujira ambao ni takriban Sh2.2 bilioni kwa mwezi na Sh73 milioni kwa siku.

Nyota Cristiano Ronaldo wa Al-Nassr. PICHA | AFP

Ronaldo, 37, alisalia mchezaji huru baada ya kuagana na Manchester United mnamo Novemba 2022 kufuatia mahojiano aliyoyatumia “kulipua kibomu” ugani Old Trafford.

Mbali na kukosoa waajiri wake, alilalamikia pia kuhangaishwa na vinara wakuu wa Man-United huku akisisitiza kuwa hana heshima yoyote kwa kocha Erik ten Hag ambaye sasa anadhibiti mikoba ya mabingwa hao mara 20 wa Ligi Kuu ya Uingereza (EPL).

Kwa mujibu wa Ronaldo wakati huo, kubwa zaidi katika matamanio yake yalikuwa “kuonja ladha ya ligi mpya ya soka katika nchi tofauti”.

“Nahisi kwamba nimeshinda kila taji ambalo nilitazamia kunyanyua katika soka ya bara Ulaya na kwamba huu ndio wakati mwafaka zaidi wa kuleta tajriba yangu kitaaluma katika kabumbu ya Asia,” akasema.

Al Nassr, ambao ni mabingwa mara tisa wa Saudi Pro League, walisema usajili wa Ronaldo ni “mwanzo wa kuwekwa kwa historia”.

“Ujio wake utazidi kuchochea ligi yetu, taifa letu na vizazi vijavyo – wavulana kwa wasichana – kufikia ubora wao katika fani ya usogora.”

Awali, Ronaldo alikuwa ametupilia mbali ofa ya kujiunga na kikosi cha Al Hilal nchini Saudi Arabia kwa Sh45.4 bilioni baada ya kusisitiza kuwa anafurahia maisha yake ugani Old Trafford alikokuwa akidumishwa kwa mshahara wa Sh74.5 milioni kwa wiki.

N’GOLO KANTE

Kiungo huyo mzoefu raia wa Ufaransa anatazamiwa kukamilisha uhamisho wake kutoka Chelsea hadi Al-Ittihad ya Saudi Arabia wakati wowote kuanzia sasa.

Kante, 32, anatarajiwa kutia saini mkataba wa miaka miwili utakaomshuhudia akipokezwa mshahara wa Sh14.8 bilioni kwa mwaka.

Baada ya kuridhisha kambini mwa Boulogne mnamo 2012, Kante alisajiliwa na Caen bila ada yoyote mnamo 2013 na akasaidia kikosi hicho kufuzu kwa Ligi Kuu ya Ufaransa (Ligue 1). Alihudumu kambini mwa Caen hadi 2015 aliposajiliwa na Leicester City kwa kima cha Sh784 milioni mnamo 2015.

Ushawishi wake uwanjani King Power ulisaidia Leicester kunyanyua taji la EPL katika msimu wa 2015-16 naye akatawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka kambini mwa kikosi hicho kilichokuwa chini ya kocha Claudio Ranieri.

Mnamo 2016, Kante aliingia katika sajili rasmi ya Chelsea kwa kima cha Sh4.5 bilioni. Aliongoza kikosi hicho kutia kibindoni ufalme wa EPL mnamo 2016-17 na akawa mchezaji wa kwanza wa katikati ya uwanja baada ya Eric Cantona mnamo 1992 na 1993 kutwaa taji la EPL kwa misimu miwili mfululizo akivalia jezi za klabu tofauti.

Kante aliwajibishwa na timu ya taifa ya Ufaransa kwa mara ya kwanza mnamo 2016 na akawa sehemu ya kikosi kilichoambulia nafasi ya pili nyuma ya Ureno kwenye fainali za Euro 2016.

Mnamo 2017, alitawazwa Mchezaji Bora wa Mwaka nchini Ufaransa, hiyo ikiwa mara ya kwanza baada ya miaka saba kwa sogora wa EPL kutia kibindoni taji hilo. Miezi 12 baadaye, alisaidia timu yake ya taifa kupepeta Croatia 4-2 na kunyanyua Kombe la Dunia kwenye fainali zilizoandaliwa nchini Urusi.

Kante aliambulia nafasi ya nane kwenye tuzo ya Ballon d’Or mnamo 2017 kabla ya kuorodheshwa wa 11 kwenye kinyang’anyiro hicho cha kuwania taji la Mwanasoka Bora Duniani mwaka mmoja baadaye. Chelsea wamekuwa wakimdumisha kwa ujira wa Sh24 milioni kwa wiki, malipo yanayowiana na kiasi ambacho hutiwa mfukoni na kipa ghali zaidi duniani, Kepa Arrizabalaga. Hadi alipotua Chelsea, alikuwa akidumishwa kwa mshahara wa Sh18 milioni kwa wiki kambini mwa Leicester.

  • Tags

You can share this post!

Enyi kina Brayo na Jayden, mkienda Lamu mtakosa majina!

Mikakati ya Azimio kuzima Mswada wa Fedha 2023 imeiva

T L