Na CECIL ODONGO
TIMU ya St Anthony Boys’ High School Kitale imetwaa taji la soka kwa kutandika Dagoretti High School 2-0 katika fainali michezo ya kitaifa ya shule za upili ikifika tamati Jumamosi.
St Anthony’s ilitwaa taji hilo ambalo ni la sita kwao baada ya kuilemea Dagoretti High School 2-0 kwenye mechi ambayo ilihudhuriwa na mashabiki wengi waliojaza uwanja wa Bukhungu.
Kiungo Alvin Kipchirchir Kibet alifungia ‘Solidarity Boys mabao hayo mawili, moja kati kipindi cha kwanza na bao jingine kipindi cha pili kuleta furaha riboribo nyusoni mwa halaiku ya mashabiki ambao bila shaka walikuwa wakiwashabikia.
Kibet ambaye anavalia nambari 10 na anapata msukumu wa kujituma zaidi kwa kumuiga nyota wa Barcelona Lionel Messi, alikuwa kipenzi cha mashabiki wengi kutokana na jinsi alivyowageuza mabeki wa Dagoretti.
Kando na kuwa ni ubingwa wa sita kwa St Anthony’s, kocha Peter ‘Big Machine’ Mayoyo ametwaa mataji 12 ya shule za upili. Mayoyo pia amewahi kushinda taji hilo na Mombasa High School.
“Mimi ndiye baba lao. Hakuna kocha hapa nchini ambaye ananifikia. Mechi hii tumeishinda na umeona jinsi ambavyo tuliwalemea wapinzani wetu. Sasa tunalenga ubingwa wa Afrika Mashariki ambao nina hakika tutauleta nchini,” akasema Mayoyo akiwa mwingi wa furaha.
Kocha wa Joseph Makokha alikiri kuwa walilemewa na wapinzani wao na akaahidi kuwa watarekebisha makosa waliyoyafanya wakati wakijiandaa kuwakilisha nchi pia kwenye michezo ya Afrika Mashariki kuanzia mnamo Ijumaa.
Katika soka ya wanawake, mabingwa watetezi Wiyeta walipoteza taji lao ambalo lilitwaliwa na Butere Girls inayonolewa na Howard Makhokha. Bao hilo lilifungwa na Judith Makokha kupitia mkwaju wa penalti.
Hali ilikuwa vivyo hivyo kwenye voliboli ambapo Kwanthanze waliokuwa wameshinda ubingwa kwa miaka sita mfululizo walilemewa 3-1 (25-19, 15-25, 22-25, 25-21) na Kesogon Mixed Secondary kutoka Trans Nzoia.
Oyugi Ogango Secondary kutoka Nyanza nao walishinda Bukokholo 54-40 kutoka Magharibi na kuibuka na ubingwa kwenye mpira wa vikabu.
Ruthimitu nao walishinda Andersen High School 3-2 (25-21, 15-25, 26-24, 20-25, 15-8) na kutwaa ubingwa wa voliboli ya wavulana.
Kinara wa Mawaziri Musalia Mudavadi, Waziri wa Elimu Ezekiel Machogu na mwenzake wa Michezo Ababu Namwamba walihudhuria fainali hizo na kuwatuza washindi.