• Nairobi
  • Last Updated June 1st, 2023 12:23 AM
UEFA: Fainali ya Man City na Chelsea kuandaliwa jijini Porto na kuhudhuriwa na mashabiki 12,000

UEFA: Fainali ya Man City na Chelsea kuandaliwa jijini Porto na kuhudhuriwa na mashabiki 12,000

Na MASHIRIKA

FAINALI ya Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) msimu huu kati ya Chelsea na Manchester City itachezewa mjini Porto, Ureno mnamo Mei 29, 2021 na kuhudhuriwa na jumla ya mashabiki 12,000; yaani 6,000 kutoka kila kikosi.

Mchuano huo ulihamishwa kutoka uga wa Ataturk Olympic, Uturuki kwa sababu ya masharti makali ya kudhibiti janga la corona katika nchi ya Uingereza iliyopiga marufuku ziara za kuingia nchini Uturuki.

Ureno ni miongoni mwa mataifa ambayo hayako katika orodha ya nchi ambazo zimepigwa marufuku na Uingereza na mashabiki wako huru kuhudhuria fainali ya UEFA bila kuhitajika kuingia karantini watakaporejea nyumbani.

“Haikuwa haki kuwanyima mashabiki fursa adimu ya kuhudhuria pambano kali la fainali ya soka ya haiba kubwa zaidi barani Ulaya. Nina furaha kwamba suluhu kwa suitafahamu iliyokuwepo imetatuliwa,” akasema raia wa Shirikisho la Soka la bara Ulaya (Uefa), Aleksander Ceferin.

Awali, kulikuwa na mapendekezo kutoka kwa vinara wa Uefa na Shirikisho la Soka la Uingereza (FA) kwa fainali hiyo kuandaliwa uwanjani Wembley, Uingereza ila mwafaka kati yao na Serikali ya Uingereza ukakosa kupatikana kwa sababu ya kanuni za karatini kwa wadhamini, wageni mashuhuri na wanahabari.

Chelsea na Man-City wamekiri kwamba wanashauriana zaidi na washikadau mbalimbali kuhusu jinsi ya kufanikisha mpango wa kutoa tiketi za mahudhurio kwa mashabiki wao.

Man-City wamefichua kwamba watadhamini usafiri wa mashabiki wao kutoka jijini Manchester, Uingereza hadi Porto, Ureno huku wakishikilia kwamba wataanza kuuza tiketi mnamo Mei 24, 2021.

Hii ni mara ya pili mfululizo kwa fainali ya UEFA kuandaliwa nchini Ureno baada ya fainali ya msimu uliopita wa 2019-20 kati ya Bayern Munich na Paris Saint-Germain (PSG) kufanyika jijini Lisbon. Bayern kutoka Ujerumani walitawazwa washindi baada ya kupiga PSG 1-0.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Maandalizi ya Idd yanoga Ramadhan ikifika tamati

Lukaku na Young watozwa faini kwa kukiuka kanuni za corona...