• Nairobi
  • Last Updated June 12th, 2024 4:24 PM
UEFA: Je, taji la Copa del Rey litaipa nguvu Real Madrid dhidi ya Manchester City?

UEFA: Je, taji la Copa del Rey litaipa nguvu Real Madrid dhidi ya Manchester City?

Na MASHIRIKA

KOCHA Carlo Ancelotti amewataka sasa masogora wake wa Real Madrid kujituma maradufu na kukamilisha kampeni za msimu huu wakiwa na mataji matatu.

Miamba hao walipepeta Osasuna 2-1 jijini Seville mnamo Jumamosi na kutawazwa wafalme wa Copa del Rey. Ilikuwa mara ya kwanza tangu 2014 kwa Real kutwaa kombe hilo ambalo wamelinyanyua mara 20 katika historia na mara tatu pekee katika kipindi cha miaka 31 iliyopita.

Real, almaarufu Los Blancos, walifunga mabao yao kupitia kwa Rodrygo Silva de Goes. Osasuna, waliokuwa wakinogesha fainali ya Copa del Rey kwa mara ya pili katika historia, walifutiwa machozi na Lucas Torro. Fainali dhidi ya Real ilikuwa fursa nzuri kwa Osasuna kujizolea taji lao la kwanza la haiba kubwa katika kipindi cha miaka 103.

Rodrygo aliweka waajiri wake kifua mbele kunako sekunde ya 106 na bao hilo likawa la haraka zaidi kuwahi kufungwa kwenye fainali ya kuwania kombe katika soka ya Uhispania tangu 2006.

Miaka 17 iliyopita, Raul Tamudo alicheka na nyavu za Real Zaragoza baada ya sekunde 44 pekee na kuchochea kikosi chao cha Espanyol kushinda Copa del Rey kwa mabao 4-1 kwenye fainali iliyochezewa ugani Santiago Bernabeu.

Real walipokeza Eintrecht Frankfurt ya Ujerumani kichapo cha 2-0 mnamo Agosti 2022 katika uwanja wa Helsinki Olympic, Finland na kujizolea taji la UEFA Super Cup.

Ni matarajio ya Ancelotti kwamba masogora wake wataelekezea macho yote kwa kipute Klabu Bingwa Ulaya (UEFA) baada ya kushindwa kuhifadhi Ligi Kuu ya Uhispania (LA Liga) msimu huu.

Kufikia sasa, Real wanakamata nafasi ya tatu kwenye msimamo wa jedwali la La Liga kwa alama 68, moja nyuma ya nambari mbili Atletico Madrid ambao pia wametandaza michuano 33.

Barcelona, wanaodhibiti kilele cha jedwali hilo kwa alama 82, watatawazwa mabingwa wa La Liga muhula huu – kwa mara ya kwanza tangu 2009 – iwapo wataangusha Espanyol ugani RCDE, Jumapili.

Baada ya kualika Manchester City leo Jumanne usiku kwa mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya UEFA, Real watapimana ubabe na Getafe katika La Liga nyumbani kabla ya kurudiana na Man-City uwanjani Etihad.

Watafunga kampeni zao za Mei ligini dhidi ya Valencia, Rayo Vallecano na Sevilla kwa usanjari huo.

“Tuna kila sababu ya kuangusha Man-City. Ushindi wa Copa del Rey unatarajiwa kutuchochea sote. Hatuna muda kabisa wa kusherehekea kuangusha Osasuna. Kazi kubwa bado inatusubiri,” akasema Ancelotti.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

  • Tags

You can share this post!

Lacazette abeba Lyon dhidi ya Montpellier katika Ligue 1

Askofu Oginde aapishwa rasmi kuongoza EACC

T L