• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 5:22 PM
UEFA: Manchester City na Real Madrid kumaliza udhia leo usiku

UEFA: Manchester City na Real Madrid kumaliza udhia leo usiku

NA MASHIRIKA

MANCHESTER, UINGEREZA

SARE ya 1-1 katika mkondo wa kwanza wa nusu-fainali ya Klabu Bingwa (UEFA) ugani Santiago Bernabeu, Uhispania, wiki jana inawapa Manchester City nafuu inaporudiana na Real Madrid uwanja wa Etihad, Uingereza, leo Jumatano usiku.

Hata hivyo, kocha Carlo Ancelotti wa Real amesisitiza haitakuwa rahisi kwa wenyeji wao leo, huku mashabiki wa Man-City wakitarajiwa kufika kwa wingi kushuhudia pambano hilo.

“Jumatano itakuwa kama fainali. Tutacheza tukilenga ushindi wa kutupeleka Istanbul, Uturuki, kucheza fainali katika uwanja wa Ataturk Olympic mwezi ujao,” alitanguliza kocha huyo mzoefu raia wa Italia.

“Tulicheza vizuri mkondo wa kwanza na tutavipiga vita vikali zaidi mechi ya marudiano,” akaongeza Ancelloti, 63.

Mwenzake Pep Guardiola wa Manchester City tayari ametoa onyo kama hilo kwa Real, kwamba watakutana na kibarua kizito Etihad, Uingereza.

Vile vile, mkufunzi huyo Mhispania ana imani masogora wake watatinga fainali ya Juni 10, akila mori kwamba huu unaweza kuwa mwaka wao kutawazwa wafalme wa UEFA kwa mara ya kwanza kabisa katika historia ya kombe hilo.

Katika mkondo wa kwanza, Man City walitoka nyuma kusawazisha dakika ya 67 kupitia kwa Kevin De Bruyne, baada ya Real kuwekwa mbele na Vinicius Junior dakika ya 36.

Msimu uliopita, timu hizi zilikutana kwenye hatua hii ya nusu-fainali Real wakiibuka washindi kwa jumla ya mabao 6-5.

Lakini itakumbukwa kwamba Man-City wamekuwa chuma moto nyumbani msimu huu; wanashikilia rekodi ya kutandaza mechi 14 bila kufungwa ugani Etihad, wakitinga magoli 49 na kufungwa saba.

  • Tags

You can share this post!

Rais Ruto afanya mabadiliko yaliyowaathiri Makatibu saba wa...

Raila akanusha kuna handisheki na Ruto

T L