Na MASHIRIKA
VIPUSA wa Uingereza walitinga fainali ya Kombe la Dunia kwa mara ya kwanza baada ya kukomoa wenyeji Australia 3-1 jijini Sydney.
Ushindi huo ulifanya Lionesses kuwa timu ya kwanza ya soka ya watu wazima nchini Uingereza kuwahi kufuzu kwa fainali ya dunia tangu 1966.
Ni matokeo yaliyoendeleza msururu wa matokeo bora ya warembo hao chini ya kocha Sarina Wiegman ambaye huu ni mwaka wake wa pili wa ukufunzi kambini mwa Uingereza. Katika msimu wake wa kwanza, Wiegman aliongoza Uingereza kutawazwa mabingwa wa Euro 20222 katika ardhi yao ya nyumbani.
Ella Toone aliwaweka Lionesses wa Uingereza kifua mbele kunako dakika ya 36 kabla ya Australia kusawazishiwa na Sam Kerr aliyepangwa katika kikosi cha kwanza kwa mara ya kwanza kwenye fainali za mwaka huu.
Hata hivyo, Lauren Hemp alirejesha Uingereza uongozini kabla ya Alessia Russo kupachika wavuni goli la tatu. Vipusa wa Wiegman watakutana sasa na Uhispania katika fainali itakayochezewa jijini Sydney mnamo Agosti 20, 2023.
Uingereza walifungua kampeni zao za Kundi D kwa ushindi wa 1-0 dhidi ya Haiti kabla ya kabla ya kupokeza Denmark kichapo sawa na hicho. Walicharaza China 6-1 katika pambano la mwisho kundini kabla ya kufunga Nigeria penalti 4-2 kufuatia sare ya tasa katika hatua ya 16-bora.
Kabla ya kung’oa wenyeji Australia, Uingereza walipepeta Colombia 2-1 katika hatua ya robo-fainali.
TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO