• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 9:50 AM
Ulinzi Starlets mbioni kutetea ubingwa wa Kombe la FKF

Ulinzi Starlets mbioni kutetea ubingwa wa Kombe la FKF

NA TOTO AREGE 

ULINZI Starlets wanapania kutetea taji lao mnamo Jumapili watakapomenyana na Nakuru City Queens katika mechi ya fainali ya Kombe la Wanawake la Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) uwanjani Nyayo jijini Nairobi.

Hili ni toleo la pili baada ya toleo la kwanza mwaka 2021 ambapo, Ulinzi walishinda taji hilo kwa kuwalaza mabingwa wa Ligi Kuu ya Wanawake ya Kenya (KWPL) Vihiga Queens 2-0 katika uwanja wa Maonyesho ya Kilimo (ASK) jijini Nakuru.

Katika mechi ya nusu fainali Jumatano wiki iliyopita, Nakuru iliilaza Kibera Girls Soccer (Divisheni ya Kwanza) 3-2 huku Ulinzi ikiilaza Kisumu All Starlets 3-0 katika Taasisi ya Sayansi na Teknolojia ya Rift Valley (RVIST) na kufuzu kwa fainali hizo.

Mkufunzi wa Ulinzi Joseph Mwanzia atakuwa anataka kuendeleza ushindi huo wa nusu fainali ili kutetea ubingwa wao nyumbani.

“Tutalazimika kupigania ubingwa, tulipoteza taji la ligi na lazima tumalize msimu na kombe. Hiyo ndiyo kazi pekee tuliyo nayo katika uwanja wa Nyayo siku ya Jumapili,” amesema Mwanzia.

Nakuru kwa upande mwingine itatarajia kuandikisha historia katika fainali hizo, baada ya kuondolewa katika robo fainali ya kinyang’anyiro hicho mwaka wa 2021 na Bunyore Starlets ambao waliwashinda 1-0 katika uwanja wa Mumboha, Kaunti ya Vihiga.

“Baadhi ya wachezaji wangu wana majeraha madogomadogo kutoka kwa mchezo uliopita, lakini watapatikana kwa uteuzi. Tuko tayari kwa kuandikisha historia,” alisema kocha mkuu wa Nakuru Chris Wesonga.

Ulinzi na Nakuru walikuwa katika fomu nzuri msimu uliopita baada ya kumaliza katika nafasi ya tatu na sita kwenye jedwali wakiwa na alama 49 na 32 mtawalia katika msimu uliokamilika wa KWPL 2022/23.

Mshambulizi wa Nakuru Elizabeth Muteshi na Melon Mulandi ambao wote walifunga bao moja dhidi ya Kibera katika nusu fainali watakuwa wachezaji wa kutazama kwenye fainali.

Kwa upande wa Ulinzi, washambulizi Fasilah Adhiambo, Mercy Airo na Joy Kinglady wataongoza safu ya mashambulizi.

Katika mechi nyingine katika uwanja huo, Kibera Girls Soccer (Divisheni ya Kwanza) itamenyana na Kisumu All Starlets kuwania nafasi ya tatu.

Mshindi ataenda nyumbani na Sh500,000 naye wa pili atapewa Sh250,000. Nambari tatu na nambari nne watapokea Sh150,000 na Sh100,000 mtawalia.

  • Tags

You can share this post!

ADAK yapiga Wakenya 20 marufuku kwa kudaiwa kutumia dawa za...

Pigo kuu Pasta Ezekiel akizuiwa kuhudhuria mkutano wa injili

T L