• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 4:31 PM
Viongozi wahimizwa kupiga jeki wanamichezo

Viongozi wahimizwa kupiga jeki wanamichezo

NA LAWRENCE ONGARO

WANAMICHEZO katika Kaunti ya Kiambu wanatoa malalamiko wakisema kukosa ufadhili ni tishio kwa vipaji vyao.

Haya yalifichuliwa kwenye kikao kimoja kilichoongozwa na Kanisa la Maranatha lililoko mjini Thika, ambalo kwa muda limekuwa likijaribu kuwaleta vijana pamoja kwa lengo la kuwafariji na kuwapa mwongozo.

Mchungaji mkuu katika kanisa hilo Bw Ephraim Muiruri amewaomba viongozi hasa wale kutoka Kaunti ya Kiambu wawajibike na kusaidia vijana wanaolenga kuimarika kwenye spoti.

“Huku kuna vijana wengi walio na talanta katika michezo mbalimbali lakini wamekosa mfadhili,” alisema mchungaji huyo.

Aliwataka maafisa wakuu wa michezo katika Kaunti ya Kiambu kuwajibika na kuhakikisha vijana wanapata misaada ya kifedha na vifaa bora vya michezo.

Mnamo mwezi Aprili 2023, kanisa hilo la Maranatha lilijumuisha zaidi ya wanamichezo 2,134, walioshiriki katika michezo tofauti katika uwanja wa michezo wa Thika.

“Mimi kama mchungaji singetaka kuona vijana wakiingilia vitendo vya uhalifu na maovu mengine katika jamii. Wakikosa fursa katika michezo huenda wakashawishika kuingilia uovu,” alisema Bw Muiruri.

Meneja wa kituo cha wanariadha eneo la Witeithie mjini Thika, Florence Wambura, aliwashutumu maafisa wa michezo katika kaunti ya Kiambu kwa kutowajibika.

Hawa maafisa hawaelewi shida wanazopitia wanamichezo. Wao hawazuru maeneo ya mashinani ili kujua shida zao. Wanastahili kuzinduka waliko ili wafahamu yanayoendelea mashinani,” alifafanua Bi Wambura.

Alisema iwapo maafisa hao wataendelea kuketi kitako bila kuzingatia maswala ya michezo, bila shaka watakusanyika wote na kufululiza hadi afisi ya Gavana wa Kiambu Kimani Wamatangi ili kuwasilisha shida zao huko.

Alisema fedha za michezo kwenye mgao wa bajeti katika Kaunti ya Kiambu zinastahili kukaguliwa ili wananchi wajue mahali zinakoenda.

Refa wa soka (mstaafu) Winston Mureithi alisema iwapo serikali inataka kumaliza maswala ya pombe haramu na dawa za kulevya, kwanza wainue hali ya michezo mitaani ili vijana wajihusishe na michezo.

Vijana wakipewa ushauri. PICHA | LAWRENCE ONGARO

Alisema ufisadi unastahili kuangamizwa katika idara ya michezo katika kaunti ili vijana wapate nafasi ya kuinuka.

Mwenyekiti wa wasanii mjini Thika Joseph ‘Lion’ Kiruhi anasema vijana wengi wamevunjika moyo kwa kutoshughulikiwa.

“Vijana wengi wana vipaji vya usanii kama uimbaji, uigizaji, ngonjera na talanta nyinginezo lakini hakuna wa kuwajali,” alisema Bw Kiruhi.

Baadhi ya michezo inayoangaziwa zaidi mashinani ni soka, riadha, netiboli, mpira wa vikapu, magongo, na urushaji vishale (darts).

Mwanamichezo wa mpira wa vikapu Dancan Kyalo anasema katika mtaa wa Ngoingwa uwanja waliotumia kwa michezo umenyakuliwa na jumba kubwa likajengwa mahali hapo.

“Tungetaka kuelezwa waziwazi ni kina nani hao wananyakua mali ya umma,” alisema Kyalo.
  • Tags

You can share this post!

Gachagua: Wakenya wasio na kazi hawatatozwa ushuru

Elimu ilivyochangia katika ustawi wa nchi tangu 1963

T L