• Nairobi
  • Last Updated February 25th, 2024 10:30 AM
Wambua ataja wanaraga sita wapya Kenya Shujaa ikielekea mawindoni Kombe la Afrika

Wambua ataja wanaraga sita wapya Kenya Shujaa ikielekea mawindoni Kombe la Afrika

NA GEOFFREY ANENE

KOCHA Kevin ‘Bling’ Wambua amejumuisha wachezaji sita wapya katika kikosi cha mwisho cha Kenya Shujaa kitakachoshiriki Kombe la Afrika la raga ya wachezaji saba kila upande jijini Harare, Zimbabwe mnamo Septemba 16-17.

Samuel Asati na Festus Shiasi (KCB), Nigel Amaitsa (Nondescripts), Patrick Odongo (Daystar Falcons), Bildad Ogeta (Menengai Oilers) na William Muhanji (Kabras Sugar) wamo mbioni kuchezea Shujaa kwa mara ya kwanza kabisa.

Wambua aliwajumuisha katik kikosi hicho kitakachosafiri Septemba 14 kushiriki mashindano hayo ya mataifa 12 yatakayotumiwa pia kuingia Olimpiki 2024 pamoja na njia ya kushiriki mchujo wa kupandishwa ngazi ya Raga za Dunia.

“Wachezaji hawa wapya walionyesha talanta ya hali ya juu na bidii kwenye raga za kitaifa zilizojumuisha duru ya Dala, Driftwood, Prinsloo, Christie, Tisap na Kabeberi Sevens,” amesema.

Wachezaji wazoefu kikosini ni manahodha Vincent Onyala na Anthony Omondi, ambao ni manahodha, pamoja na George Ooro, John Okoth, Brian Tanga na Kevin Wekesa.

Shujaa wako Kundi B pamoja na Nigeria, Nambia na Zambia. Afrika Kusini, Madagascar, Tunisia na Ivory Coast wamekutanishwa katika Kundi A nao mabingwa watetezi Uganda watachapana na Zimbabwe, Burkina Faso na Algeria katika Kundi C.

Wambua anasaidiwa na makocha Louis Kisia na Andrew Amonde, mnyooshaji wa viungo Lamech Bogonko naye Steven Sewe ni meneja wa timu.

  • Tags

You can share this post!

ODM yazimwa kufuta jina la seneta Ojienda kwenye rejista

Wafanyabiashara wajenga vibanda visivyotakikana wakidai...

T L