• Nairobi
  • Last Updated April 15th, 2024 2:58 PM
Wanasoka wa Brazil wafuzu kwa robo-fainali za Olimpiki huku Ujerumani wakiaga kipute hicho

Wanasoka wa Brazil wafuzu kwa robo-fainali za Olimpiki huku Ujerumani wakiaga kipute hicho

Na MASHIRIKA

MABINGWA watetezi Brazil waliingia hatua ya robo-fainali za soka ya Olimpiki kwa wanaume kirahisi mnamo Julai 28, 2021 huku Ujerumani walioridhika na nishani ya fedha mnamo 2016 wakidenguliwa.

Fowadi matata wa Everton, Richarlson Andrade alipachika wavuni mabao mawili mwishoni mwa kipindi cha pili na kusaidia Brazil kusajili ushindi wa 3-1 dhidi ya Saudi Arabia na kukamilisha kampeni za Kundi D kileleni. Ivory Coast waliambulia nafasi ya pili baada ya kulazimishia Ujerumani sare ya 1-1.

Katika Kundi B, Korea Kusini waliwapepeta Honduras 6-0 na kufuzu kwa hatua ya nane-bora wakiwa kileleni. New Zealand walikamata nafasi ya pili kutokana na uchache wa mabao baada ya kutoka sare tasa na Romania.

Brazil waliwekwa kifua mbele na Matheus Cunha mwanzoni mwa kipindi cha kwanza kabla ya juhudi zake kufutwa na Abdulelah Al-Amri aliyesawazishia Saudi Arabia uwanjani Saitama.

Richarlson aliyefunga mabao matatu katika mchuano wa ufunguzi wa Kundi D na kusaidia Brazil kushinda Ujerumani 4-2, alicheka na nyavu za Saudi Arabia katika dakika ya 76 kabla ya kufunga goli jingine sekunde chache kabla ya mchezo kutamatika.

Ujerumani walihitajika kupepeta Ivory Coast ili kufuzu. Hata hivyo, matumaini yao yalizamishwa katikati ya kipindi cha pili baada ya Benjamin Henrichs kujifunga kabla ya Eduard Loewen kusawazisha mambo dakika sita baadaye.

Timu zote za Kundi B zimefuzu kwa raundi ya mwisho kila moja ikiwa na alama tatu. Hata hivyo, ni Korea Kusini waliosonga mbele wakidhibiti kilele cha jedwali baada ya mabao matatu kutoka kwa Hwang Ui-jo kuwasaidia kucharaza Honduras 6-0. Watamenyana sasa na New Zealand katika hatua ya robo-fainali.

TAFSIRI NA: CHRIS ADUNGO

You can share this post!

Amonde astaafu kuchezea Kenya Shujaa ikimakiza ya tisa...

Pombe haramu lita zaidi ya 300 yaharibiwa katika mitaa...