• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:03 PM
Wasichana 4 wa Taita Taveta wapata udhamini wa mafunzo ya riadha

Wasichana 4 wa Taita Taveta wapata udhamini wa mafunzo ya riadha

NA ABDULRAHMAN SHERIFF

WASICHANA wanne, watatu wanafunzi wa shule za upili na mwingine wa shule ya msingi kutoka Kaunti ya Taita Taveta, wamebahatika kupata udhamini wa masomo pamoja na kambi ya mafunzo ya mchezo wa riadha iliyoko mjini Kimana, Kaunti ya Kajiado.

Wanafunzi hao, Agnes Mwashigadi, Jardeen Malemba na Phelice Malemba wa shule za sekondari na Maria Shali anayesoma shule ya msingi wamepata udhamini huo kutoka kwa shirika lisilokuwa la serikali la Rainbow of Magnolia Fountains of Life.

Shirika hilo linaloongozwa na mwanzilishi wake Dariusz Stuj, raia wa Marekani na Mkurugenzi, Robert Saruni, limewapatia shule za mabweni wasichana hao ambao watasoma hapo Kimana na wakati huo huo kupata mafunzo ya mchezo wa riadha.

Chipukizi hao watakaojumuika na mwenzao Josephine Sempeyu, mwanafunzi wa shule ya msingi ambaye atashiriki mbio za mita 1,500 jijini Nairobi mwezi ujao za kupigania nafasi ya kuwa katika timu ya taifa ya vijana itakayoshiriki mashindano ya Riadha ya Dunia.

Wasichana wanne kutoka Kaunti ya Taita Taveta wakiwa na mdhamini wao Dariusz Stuj hapo Kimana, Kaunti ya Kajiado. Picha/Abdulrahman Sheriff

Mashindano hayo ya riadha ya dunia yatafanyika Nairobi mwezi wa Agosti. Wasichana hao watapata mafunzo kutoka kwa mwanariadha Boniface Wambua ambaye ameshiriki mbio kadhaa nchini na ng’ambo.

Saruni amesema wasichana hao walionekana na kocha Wambua wakati wa mbio za nyika za jimbo la Pwani zilizofanyika Wundanyi mwezi wa Februari ambapo wote walifuzu kuwakilisha Pwani kwenye mbio za nyika za kitaifa zilizokuwa Nairobi mwezi huo.

“Tunataka kukuza vipaji vya wasichana hawa ili miaka ijayo wawe wanariadha wa kutajika. Tunasisitiza zaidi juu ya masomo yao kwani kuna umuhimu wao pia kuwa na mafanikio katika masomo yao,” akasema mkurugenzi huyo.

Wakuu hao wa Rainbow walikutana na wazazi wa wasichana hao wanne Ijumaa iliyopita na kukubaliana mambo kadhaa yakiwemo wawe wanaishi katika kambi itakayosimamiwa na wanawake nyakati shule zikiwa zinafungwa kwa siku chache.
Wameanzisha kambi hiyo kusaidia wanariadha kutoka familia zisizojiweza ambazo hazina uwezo wa kulipa kambi zinazotoza malipo. Wataanza kujiunga na mradi huo zitakapofunguliwa shule kwa muhula mpya mwishoni mwa Julai.

You can share this post!

Mfanyabiashara Chris Kirubi afariki akiwa na umri wa miaka...

Majaji waliotemwa na Uhuru hatimaye wazungumza