• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Yego kuwinda tiketi ya dunia Omanyala akiahidi kutimka chini ya sekunde 10 Kasarani

Yego kuwinda tiketi ya dunia Omanyala akiahidi kutimka chini ya sekunde 10 Kasarani

Na AYUMBA AYODI

MSHINDI wa nishani ya shaba ya Riadha za Dunia, Rhonex Kipruto na bingwa wa Afrika wa kurusha mkuki Julius Yego sasa watashiriki mashindano ya kuchagua timu zitakazoshiriki Riadha za Dunia na michezo ya Jumuiya ya Madola yatakayoanza ugani Kasarani, Ijumaa.

Wakati huo huo, mfalme wa Afrika mbio za mita 100 Ferdinand Omanyala analenga kutimka umbali huo chini ya sekunde 10 uwanjani Kasarani.

Kipruto hakuwa amejumuishwa katika orodha ya watimkaji watakaoshiriki fainali ya mbio za mita 10,000 Jumamosi saa saba unusu mchana. Rais wa Shirikisho la Riadha Kenya (AK) Jackson Tuwei alisema Jumatano kuwa walikuwa wakichunguza masuala fulani kabla ya kumruhusu Kipruto kushiriki.

Yego, ambaye alitwaa ubingwa wa kurusha mkuki zaidi ya siku 10 zilizopita mjini Reduit, Mauritius, sasa ana fursa ya mwisho kujaribu kufuzu kushiriki Riadha za Dunia.

AK haikuwa imejumuisha fani za uwanjani katika mashindano ya kuchagua timu ya taifa, lakini sasa imeongeza mchezo wa kinadada wa ‘Hammer’ na urushaji wa mkuki upande wa wanaume. Fani hizo zitafanyika Ijumaa na Jumamosi mtawalia.

Riadha za Dunia ni Julai 15-24 katika jimbo la Oregon, Amerika nayo michezo ya Jumuiya ya Madola ni Julai 28 hadi Agosti 8 mjini Birmingham, Uingereza.

Yego, ambaye aliandikisha historia kwa kushinda taji la dunia mwaka 2015 nchini Uchina, alikuwa ametunukiwa tiketi ya michezo ya Jumuiya ya Madola kwa sababu hajarusha mkuki umbali wa kuingia Riadha za Dunia wa mtupo wa mita 85.

Mtupo wake bora msimu huu ni mita 79.62 alioandikisha akishinda taji la Afrika mjini Reduit.

Omanyala, ambaye ametimka mita 100 chini ya sekunde 10 mara tatu humu nchini, ameratibiwa kuchana mbuga Jumamosi saa tisa kasoro dakika 20 alasiri katika mbio za kufunga mashindano haya yaliyovutia wanariadha 185.

Omanyala alikimbia sekunde 9.77 akiweka rekodi ya Afrika akikamilisha makala ya 2020 ya Kip Keino Classic katika nafasi ya pili. Alinyakua taji la Kip Keino Classic mwezi uliopita kwa sekunde 9.85.

“Mkazo wa upande wa kushoto wa tumbo langu niliokuwa nao nilipotimka mita 200 kwenye Riadha za Afrika haupo tena na Wakenya wawe tayari kuona maonyesho ya kusisimua kutoka kwangu,” alisema Omanyala akifanya mazoezi ya mwisho chini ya kocha wake Duncan Ayiemba uwanjani Kasarani.

Omanyala, ambaye pia aliongoza Kenya kutawala mbio za mita 100 kupokezana vijiti (4x100m) mjini Reduit, ataonana uso kwa macho na walioshirikiana naye Mike Mokamba, Dan Kiviasi na Samuel Imeta.

Omanyala na mkazi wa Amerika Moitalel Mpoke, ambaye hutimka mbio za mita 4oo kuruka viunzi, ni washiriki pekee wa mbio fupi ambao wamefuzu kushiriki Riadha za Dunia.

Vita vikali vinatarajiwa kushuhudiwa katika mbio za mita 800 wanaume ambapo kuna Emmanuel Korir na Ferguson Rotich walioshinda medali tya dhahabu na fedha kwenye Olimpiki mwaka jana. Pia kuna bingwa wa dunia riadha za Under-20 Emmanuel Wanyonyi, ambaye ametetemesha kwenye Diamond League mjini Rabat na duru za Continental Gold Tour za Kip Keino Classic na Golden Spike Ostrava. Noah Kibet, ambaye aliambulia medali ya shaba kwenye Riadha za Dunia za Under-20 mwaka 2021 na kupata fedha kwenye Riadha za Dunia za Ukumbini, pia yuko kwenye orodha ya mita 800.

Malkia wa dunia mbio za mita 5,000 Hellen Obiri ameamua atatimka mbio za mita 10,000 pekee Ijumaa. Hata hivyo, lengo lake ni kutetea taji la dunia mita 5,000 na kisha kuamua mbio gani kati ya hizo mbili atatimka kwenye michezo ya Jumuiya ya Madola.

Baadhi ya wapinzani wake katika mita 10,000 ni bingwa wa mbio za nyika duniani mwaka 2017 Irene Cheptai, malkia wa Afrika mita 5,000 Caroline Nyaga na mshindi wa nishani ya fedha ya dunia Margaret Chelimo pamoja na Sheila Chepkirui.

TAFSIRI: GEOFFREY ANENE

  • Tags

You can share this post!

Wamiliki hoteli waelezea hofu kuhusu Covid-19

CR7 achoka United, ataka kwenda zake

T L