Microsoft kushirikiana na vyuo vikuu kuvumisha teknolojia

Microsoft kushirikiana na vyuo vikuu kuvumisha teknolojia

Na BERNARDINE MUTANU

Kampuni ya kutengeneza kompyuta ya Microsoft itaingia katika ushirikiano na vyuo vikuu na taasisi za mafunzo kukuza matumizi ya teknolojia katika elimu.

Ushirika huo utawezesha vyuo na taasisi za mafunzo kutekeleza vyema matumizi ya teknolojia katika elimu.

Hatua ya Microsoft inasemekana kuwa juhudi zake za kukita mizizi nchini. Hatua hiyo pia inalenga kukuza wataalam watakaochukua mfumo wa dijitali katika viwango vipya katika sayansi, maarifa ya kidijitali na mawanda mengine ya utafiti.

Maafisa kutoka taasisi zilizochaguliwa watapewa mafunzo na Microsoft ili kuwa na uwezo wa kuziba nyufa zilizopo, kuwezesha wanafunzi kuondoka vyuoni wakiwa na uwezo mkuu zaidi wa kuajiriwa au kujiajiri.

Microsoft tayari imetia sahihi mkataba wa makubaliano na Chuo Kikuu cha Mt Kenya, moja ya washikadau wake katika mradi huo.

“Mkataba huo ni utaratibu mpana wa ushirikiano kati ya mashirika ya umma na mashirika ya kibinafsi ili kuwezesha mabadiliko mema katika utoaji na upokeaji mafunzo,” alisema Anthony Salcito, makamu wa rais wa Worldwide Education, mpango wa Microsoft Corporation.

Naibu Chansela wa MKU Stanley Waudo alisema mpango huo utafaa sana wanafunzi wa programu wazi za masomo chuoni humo. Utasaidia pia kuvutia wanafunzi wapya na kuhifadhi walioko.

“Tuna zaidi ya wanafunzi 16,000 katika mpango huo. Operesheni zetu za chuo pia zimerekodiwa katika mifumo ya teknolojia, ushirika huo pia utatusaidia kuimarika zaidi katika mfumo wa ICT,” alisema Prof Waudo.

You can share this post!

Uchukuzi wa BRT watengewa Sh5.5 bilioni

UBABE: Google yaizima Huawei kutumia huduma za Android na...

adminleo