Michezo

Mienendo ya mashabiki EPL: Everton ni walevi, Man U ni wavutaji sigara huku wa Liverpool wakilemewa na madeni

May 13th, 2018 1 min read

Na GEOFFREY ANENE

EVERTON ndiyo klabu iliyojaa mashabiki walevi kwenye Ligi Kuu ya Uingereza nayo Manchester United ina inaongoza orodha ya mashabiki wanaovuta sigara katika ligi hiyo ya klabu 18, utafiti unaonyesha.

Nayo Liverpool ni nambari moja katika orodha ya mashabiki walio na madeni.

Utafiti huo uliofanywa na tovuti ya FootballTips.com unaonyesha kwamba mashabiki wa Everton hunywa tembo glasi 43 kwa wiki. Mashabiki wa Crystal Palace na Chelsea wanafuata katika nafasi za pili na tatu kwa unyuaji wa tembo wakibugia glasi 40 na 35 kila wiki, mtawalia.

Wafuasi wa Tottenham wanashikilia nafasi ya nne kwa glasi 34 kila wiki, huku wale wa Manchester United, Stoke City, Burnley, Manchester City, Liverpool na Arsenal wakifunga 10-bora kwa glasi 31, 30, 26, 25, 23 na 21, mtawalia.

Mashabiki wa Southampton (glasi sita), Brighton (sita), Bournemouth (tano) na Leicester City (nne) wanakunywa kiasi cha chini cha mvinyo katika orodha ya mashabiki ambao timu zao zinashiriki Ligi Kuu ya Soka ya Uingereza ya msimu 2017-2018.

Utafiti huu uliohusisha kuhojiwa kwa mashabiki 2,400 walio na umri wa miaka 18 na zaidi ulionyesha kwamba Manchester United ina wavutaji wengi sugu wa sigara.